Atoa maagizo ujenzi Hospitali Pangani
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ametoa siku saba kuanza kwa ukarabati wa majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani.
Ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara katika hospitali hiyo na kupewa taarifa kuwa tayari serikali kuu imepeleka kiasi cha Sh mil 900 kwa ajili ya ukarabati wa majengo katika hospitali hiyo.
Amesema kuwa wananchi wanahitaji kupata huduma katika mazingira mazuri, hivyo haoni sababu za ucheleweshaji wa ukarabati huo wakati fedha tayari zipo.
“Nataka ukarabati uanze mara moja, ndani ya wiki moja na muhakikishe fedha zinatosha na ukarabati unakamilika, na kusitokee ubadhirifu wa aina yoyote ule katika mradi huu, “amesema Kindamba.
Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah kuwasimamia kwa karibu kitengo cha manunuzi, ili mradi huo usiwe na kasoro na ukamilike kama ilivyotarajiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah amesema kuwa changamoto kubwa waliyokuwa nayo ni miradi mingi kutokamilika kwa wakati, huku fedha zilizotengwa zikiwa zimeisha.
“Tuna changamoto ya miradi yetu mingi kutokamilika kwa wakati, huku mingine ikiwa fedha zimeshatumika zote, lakini na mingine ni viporo ya muda mrefu,”amesema DC huyo.