Atoa mtazamo katiba mpya, aeleza sababu kutofukuza wabunge 19

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema anaendelea kuwaacha wabunge 19 wanaodaiwa kufukuzwa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa sababu analinda haki ya yeyote kama alivyoapa. Dk Tulia alisema hayo Dodoma jana asubuhi wakati akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na kituo cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alisema anafahamu wabunge hao wamefukuzwa na chama chao lakini kesi yao iko mahakamani wakitafuta haki.

“Kisheria kwanza suala lao liko mahakamani, kikatiba ukiacha Mwanasheria Mkuu wa serikali sisi wote tumeletwa na vyama vyetu bungeni, sasa kati ya sifa unazopoteza kuwa mbunge ni pamoja na kutokuwa mwanachama wa chama fulani ama kufukuzwa au wewe mwenyewe kujitoa kwenye chama husika ukishapoteza sifa ya chama fulani unaondoka bungeni, kwa hawa 19 kuvuliwa kwao uanachama wao wanabishana na chama chao kwamba ‘mmetuvua uanachana si haki’,” alisema Dk Tulia.

Alisema kuna watu wanasema kwa nini asiwaondoe mbona mtu akiwa amehukumiwa akakata rufaa anaendelea kuwa jela hakai nje. Dk Tulia alisema kesi ya wabunge si ya jinai, ni ya kisiasa inayowahusu wao na Chadema.

“Nimeshaambiwa nimepata barua kutoka kwenye chama chao hiyo ni kweli, wakati huohuo nimepata barua kutoka kwa wabunge wenyewe wakisema kwamba ‘sisi tumeshaenda mahakamani’ sasa mimi kama mwanasheria utaratibu wa kisheria kuna misingi ambayo inafuatwa,” alisema.

Alitoa mfano wa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) waliovuliwa ubunge mwaka 2018 baada ya kufukuzwa kwenye chama hicho lakini baadaye mahakama iliwaona hawana hatia. “Mwaka jana 2022 Agosti Mahakama Kuu imetoa hukumu kwamba hawakuondolewa kwa haki, inamaanisha hawawezi kuja bungeni kwa miaka miwili waliyopoteza hawawezi kulipwa pesa kwa miaka miwili waliyopoteza, walishakuja wabunge wengine wameshalipwa,” alisema Dk Tulia.

Alisema hafahamu mahakama itatoa uamuzi gani katika kesi ya wabunge 19 hivyo anausubiri kwa kuwa ameapa kulinda katiba hivyo analinda haki ya yeyote.

Wabunge ambao Chadema imewavua uanachama ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Anatropia Theonest, Stella Flao, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Katiba mpya Kuhusu mchakato wa katiba mpya alisema iliyopo inaweza kuendelea kutumika kwenye uchaguzi ujao na kama itakuwa lazima ifanyiwe mabadiliko baadhi ya vifungu basi inawezekana.

“Nishaonana na watu wachache ukiacha wanasiasa unamuuliza unatamani kuwepo na nini kwenye katiba mpya anakwambia mpya tu unajua hii ni ya zamani, uchaguzi ujao uwe na katiba mpya ukiwa na jambo gani jipya, sio mpya tu,” alisema Dk Tulia.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button