Atoa pikipiki kwa polisi anayetumia baiskeli kuelimisha vijijini

MOROGORO: MKAZI wa Kijiji cha Kikweta, Kata ya Lumemo, Halmashauri ya Mji Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Petronila Ngurukila ametoa msaada wa  pikipiki moja  aina ya Houjue kwa Polisi Kata ya Lumemo anayetumia usafiri wa baiskeli kwa ajili ya kutoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa wananchi wa vijijini ili kurahisishia utendaji wake wa kazi.

 

Ngurukila ambaye ni mfanyabiashara katika kijiji hicho alikabidhi pikipiki hiyo kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Alex Mkama kwenye halfa iliyofanyika jana katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero kilichopo mjini Ifakara.

 

Polisi Kata wa Kata ya Lumemo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Edwin Kipimo, kwa mura mrefu alikuwa anatumia usafiri wa baiskeli kwa ajili ya kwenda kutoa elimu kwa wananchi  wa vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo.

 

 

Katika majukumu  yake hukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo  ugumu wa kuwafikia wananchi kwa wakati kutokana hali ya kijiografia na ukubwa wa Kata hiyo.

Kwa mujibu wa  matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kata ya Lumemo ina idadi ya watu 16,893 kati yao, wanaume 8,379 na wanawake 8,514 na uwiano wa kijinsia ni 98, idadi ya kaya 4,685 na wastani wa idadi ya watu katika kaya ni 3.6.

 

Hivyo, Mwananchi  huyo, alisema  amefikia uamuzi wa kutoa msaada wa  pipikipi mpya kutokana na mazingira aliyokuwa akifanya ya kutumia baiskeli kuwafikia walengwa,  na kuunga mkono juhudi na jitihada za Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu.

 

“Kuna tukio moja lilikuwa gumu katika Kijiji ninachoishi nikampigia simu Polisi Kata kwa ajili ya  kutupa msaada lakini alichelewa kufika nikamuuliza vipi mbona hufiki akasema nipo hapa kwenye msitu nakuja, alipofika nikamuona anatokea na Baiskeli,” amesema Ngurukila

 

“…. nikamuuliza Afande usafiri uko wapi akajibu huu ndio usafiri wangu, nilisikitika sana nakuona kuna umuhimu wa kuwasaidia Polisi wetu,” amesisitiza Ngurukila  mbele ya Kamanda wa Polisi wa mkoa.

 

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa , Mkama , alimshukuru mwananchi huyo kwa msaada huo na kumpongeza Mkaguzi Msaidizi, Kipimo, kwa kufanya kazi inayoigusa jamii kiasi cha kuguswa na kupata msaada huo.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Kipimo, amempongeza mwananchi huyo na jamii ya Kata ya Lumemo na kuahidi kuitunza na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Mapema mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, alisema lengo la Serikali ni kulipeleka Jeshi la Polisi karibu na wananchi, ambapo kila Kata itakuwa na askariwasomi katika ngazi ya nyota moja ikiwa ni dhamira ya kusogeza huduma kwa jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button