Atozwa faini Sh Mil 10 kujiwasilisha mtandaoni kama Rais Samia

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu Mkazi wa Mwanza, Nickson Mfoi (20), kulipa faini ya Sh milioni 10 au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili ikiwemo kujiwasilisha mtandaoni kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu.

Hukumu hiyo ilisomwa mahakamani hapo leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ashura Mnzava na mshtakiwa aliwakilishwa na Wakili wa utetezi Mwanahamisi Kiloko.

Awali Wakili Mnzava aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, lakini kabla ya kufanya hivyo mshtakiwa aliomba kukumbushwa mashtaka na alipokumbushwa alikiri na baadaye hakimu alimtia hatiani.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Kabate alisema alitoa adhabu hiyo kwa kuzingatia uzito wa makosa aliyoyafanya sambamba na matakwa ya sheria ya kanuni ya adhabu.

“Kifungu cha 369(1) na kifungu cha 75 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu kinatupa adhabu ya miezi 12, kwa sababu hakina chaguo la faini tunakwenda kifungu cha 75 na kwa shtaka la Pili sheria iko wazi, ni faini si chini ya Sh milioni 6,” alisema hakimu Kabate.

“Ukiangalia jina alilotumia kujiwasilisha siyo la kawaida, ni Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, ukimtaja Mheshimiwa Rais, umetaja Tanzania, hatuwezi kuchukulia kirahisi ni lazima uadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema.

“Kwa  shtaka ka kwanza nakuhukumu kulipa faini ya Sh milioni tano au kifungo cha miezi 12. Kwa shtaka ka pili nakuhukumu kulipa faini milioni tano au kwenda jela miezi 12. Adhabu hizi zinakwenda sambamba, ukishindwa kulipa faini utakwenda jela miezi 12, naamini ukimaliza utakuwa umejifunza,” alimaliza kusema.

Kabla ya hukumu Wakili Mnzava aliiomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria hasa ukizingatia kuwa kumekuwa na ongezeko la vitendo vya makosa ya mtandaoni katika siku za karibuni, jambo ambalo Hakimu Kabate alilikazia wakati wa kusoma hukumu yake.

Katika maombolezo yake, mshtakiwa aliiomba mahakama impe adhabu ya kifungo cha nje kwa kuzingatia kuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza na hakujua madhara ya makosa yake wakati anayafanya.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ilidaiwa  Spetemba 22, 2021 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya ulaghai na udanganyifu Mfoi alijiwasilisha mtandaoni kama Rais Samia Suluhu Hassan na kujipatia fedha jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikutwa akimiliki na kutumia laini ya simu iliyo katika umiliki wa mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma, laini ambayo ndiyo aliitumia kutenda kosa la kwanza.

Habari Zifananazo

Back to top button