JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Joyce Matingo (26) mkazi wa Unyamwanga, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo ni la Januari 8 mwaka huu saa 12:00 jioni.
Alisema siku hiyo mtuhumiwa alimfunga kamba mikono na miguu mtoto huyo, Emily mwenye umri wa miaka tisa na kuanza kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake.
Kuzaga alisema mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Unyamwanga wilayani Rungwe, alituhumiwa kuiba Sh 16,000 awamu ya kwanza na Sh 40,000 awamu ya pili zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya nyumba wanayoishi.
Alitoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kutoa adhabu zilizopitiliza na kusababisha madhara.