Aua mke, ajinyonga kwa kilemba

KIGOMA;  Rashidi Hussein Mkayaga mkazi wa Mtaa Gemu, Kata ya Mwanga Kusini Manispaa ya Kigoma Ujiji, amejinyonga kwa kutumia kilemba cha kiume cha kuvaa kichwani, muda mfupi baada ya kumuua mke wake Bernadeta Cosmas kwa kumnyonga shingo hadi kufa kwa kile kinachodaiwa ni mgogoro baina ya wanandoa hao.

Mwenyekiti wa Mtaa Gemu, Buswalu Mkama  akizungumzia na waandishi wa habari eneo la tukio, amedai chanzo  ni mgogoro wa muda mrefu na kwamba mwanamke huyo aliwahi kufika kwake na kutoa taarifa ya vitendo vya mume wake kuchukua vitu vya ndani na kuuza na mara kadhaa kesi hizo alizisuluhisha.

Pia Mwenyekiti huyo amedai siku moja kabla tukio, mwanamke huyo alilala nyumbani kwake baada ya kukimbia kwa mumewe kufuatia kipigo alichopata na kwamba alinusurika kuuawa baada ya kukabwa shingo na waya wa umema, lakini alipopata nafasi ya kuchomoka alikimbilia kwake, kulipopambazuka alifuatwa na kaka yake aitwaye Isack Cosmas.

Kwa upande wake Isack amesema siku ya tukio asubuhi alipigiwa simu na dada yake akimtaka afike kwake, hata alipomueleza angefika baadaye kwani alikuwa na kazi nyingi, lakini alimsisitiza aende muda huo.

Kutokana na msisitizo huo anasema alilazimika kuacha shughuli zake na kwenda kumuona na kumkuta kwa Mwenyekiti wa Mtaa na kuelezwa kilichokea ikiwemo kipigo, hivyo dada yake alimueleza kwamba wakati wa ugomvi wao alimtaka mumewe ampe talaka yake, hivyo akamshauri waende polisi kwenye dawati la jinsia.

Anasema akiwa na dada yake walifika nyumbani kwa shemeji yake na wakazungumza kuhusu ugomvi huo, ambapo Rashidi aliahidi kwamba mgogoro umeisha na yupo tayari kuishi na mke wake, hivyo Isack aliondoka akiwaacha wana ndoa hao nyumbani kwao.

Hata hivyo anasema jioni alipiga simu ya dada yake, lakini ilikuwa ikiita bila majibu, hivyo ilipofika saa moja usiku akaamua kwenda katika nyumba ya wana ndoa hao na kukuta mlango ukiwa umefungwa na kufuli hivyo aliondoka.

Anasema ilipofika saa tano usiku alirudi tena na kukuta mlango umefungwa, lakini mtoto waliyekuwa wakiishi naye alikuwa kwa Mwenyekiti kwa maelezo ameambiwa hivyo na baba yake.

Isack anasema kuwa asubuhi alifika kwa dada yake lakini hakukuwa na dalili za watu na kwa kushirikiana na polisi walivunja mlango na kukuta maiti za watu hao wawili ndani.

Uchunguzi wa awali wa tukio hilo unaonyesha kuwa Rashidi Hussein alimnyonga mke wake kwa mikono hadi kumuua na baadaye kutoka nje, ambapo alifunga mlango kwa nje na kurudi ndani kupitia dirishani, ambapo alifunga milango yote na madirisha na yeye kujinyonga kwa kitambaa cha kichwani.

Habari Zifananazo

Back to top button