Auawa baada ya kutishiwa na mpenzi wake

ELIZABETH Ngaza mkazi wa Mtaa wa Viwege, Kata ya Majohe, Dar es Salaam, amekutwa ameuawa, ikiwa ni siku chache baada ya kudaiwa kutishiwa na mpenzi wake chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.

Akizungumza na Daily News Digital, mama mzazi wa Elizabeth amedai licha ya kuuawa, lakini pia hawakumkuta na nguo mwilini na kwamba wanaamini ameuawa, kwani tukio limetokea siku chache baada ya kutishiwa kufanyiwa vitendo vibaya na mpenzi wake.

Amedai karibu siku tano hawakuwa wameona, lakini usiku wa kuamkia Jumamosi alikuwa na tenda ya kupika katika shule moja maeneo ya huko, hivyo wenzake wakaenda kufuata funguo nyumbani kwake na ndipo walipogundua tukio hilo.

Naye Mjumbe wa Mtaa wa Viwege, Daudi James amesema alipokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa marehemu, kuhusu mwanaume aitwaye Michael maarufu kwa jina la Pepe kwamba anamtishia maisha.

“Malalamiko ni ya muda mrefu, Aprili 15,  2024, Elizabeth alikuja serikali ya mtaa kutoa malalamiko hayo, nikamuandikia barua ya kweneda Polisi, hata majirani wanafahamu hilo, hata yule bwana nilikutana naye na kumweleza na akasema amenielewa,” amesema James.

Mtoto wa Marehemu, aitwaye Ester amesema mama yake hakuwa na tatizo lolote la kiafya kwa siku za karibuni wala ugomvi na majirani

Akifafanua ndugu wa marehemu, Rehema Ngaza amesema kwa namna walivyokuta mwili ulivyo wanaamini ndugu yao amefanyiwa vitendo vya kikatili vilivyosababisha kifo.

“Hakuwa na ugomvi na mtu zaidi ya huyo mume wake,  jamaa alikuwa hataki waachane, ” amedai Rehema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button