Auawa kwa kujihusisha na uhalifu Katavi

MTOTO wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 15 katoka Kata ya Shanwe Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ameuawa na watu wenye hasira kali akituhumiwa kujihusisha na kundi la kihalifu lijulikanalo kwa jina la ‘Damu chafu’ inasemekana mara kadhaa amekuwa akijihusisha na matukio ya uhalifu.

Maiko Chapa ameuawa na watu wasiojulikana huku ikielezwa kuwa ni moja wa watu wanaojihusisha na kundi la damu chafu ambapo kundi hilo limekuwa tishio kwa wananchi hasa nyakati za usiku ambapo wananchi kwa pamoja wamesema mbali na kutokea kwa kifo hicho lakini matukio ya uhalifu yamekithiri.

Baba wa marehemu, Titus Chapa

Titus Chapa ni baba wa marehemu kwa upande wake amesema kijana wake amekuwa akituhumiwa kutenda matukio ya uhalifu ndani ya jamii huku akieleza namna alivyokuwa akiishi naye japo kijana huyo alikuwa mara kadhaa ni mkaidi kwa baba yake kwa kutofuata maelekezo ya namna bora ya kuishi.

Kabambi Zackaria ni mwenyekiti wa Mtaa wa Kivukoni ambako tukio hilo limetokea mbali na kukiri kutokea kwa tukio hilo lakini pia amewaasa wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuwalinda watoto ili kuepukana na tuhuma za matukio ya kiuhalifu.

Mwenyekiti Mtaa wa Kivukoni,Kabambi Zackaria

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ally Hamad Makame amethibitisha kutokea kwa tukio hilo japo hakuweza kulizungumzia kwa kina akidai yuko safarini kikazi.

Hata hivyo mwili wa marehemu Maiko tayari umezikwa katika makaburi ya Kivukoni Manispaa ya Mpanda huku wananchi wakiomba Serikali kuingilia kati kwani matukio ya kihalifu na watu kujeruhiwa yamezidi katika mtaa huo.

Damu Chafu ni kundi la kihalifu la vijana wadogo walio chini ya umri wa miaka 18 ambao mara kadhaa wamekuwa wakiripotiwa kwa kufanya matukio mbalimbali ya unyang’anyi na ubakaji mkoani Katavi kwa kutumia silaha za jadi zikiwemo visu ,viwembe na nyingine na kuwajeruhi baadhi ya watu.

hivi karibuni ACP Makame aliwataarifu waandishi wa Habari kuwa kupitia misako na doria lilifanikiwa kuwakamata vijana 15 na kuwafikisha Mahakamani huku baadhi yao wakihukumiwa kulipa faini ya shilingi elfu hamsini.

Habari Zifananazo

Back to top button