Auawa kwa risasi akishambulia askari kwa mishale

MKAZI wa Kitongoji cha Manyata wilayani Chemba, Nada Songo amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa risasi maeneo ya kifuani na mguu wa kulia huku askari na mgambo wakijeruhiwa kwa mishale.

Tukio hilo lilitokea Jumapili katika Kitongoji cha Manyata, Kijiji cha Chioli kilichopo Tarafa ya Goima wilayani Chemba mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alisema Songo alifariki dunia papo hapo baada ya kushambuliwa na askari wakati akiwashambulia askari hao kwa mishale inayodhaniwa kuwa na sumu.

“Songo aliwashambulia askari hao kwa mishale wakati akikaidi kukamatwa kuhusiana na kosa ambalo alikuwa anatuhumiwa nalo la kutishia kuua kwa silaha za jadi ambazo ni mishale,”  alisema.

“Agosti 27 askari polisi walikwenda kufanya ukamataji lakini mtuhumiwa alitoroka na kukataa amri halali ya kukamatwa kuhusiana na makosa yake,” alisema.

Alisema Agosti 28 mwaka huu, askari polisi walipata taarifa ya kurejea kwa mtuhumiwa huyo huku akiendelea kutishia usalama wa watu wa kitongoji hicho.

“Askari walipokwenda kumkamata aliwashambulia kwa kutumia mishale inayodhaniwa kuwa ya sumu na kumjeruhi askari namba H 9377 PC William tumboni upande wa kushoto na askari wa akiba aitwaye Madodo Juma ambaye amejeruhiwa kwa mshale mguu wa kulia,” alisema.

Alisema eneo la tukio imekutwa mishale 23, upinde mbili, visu viwili, ala ya kuwekea mishale, dawa mbalimbali za kienyeji, hati ya kumaliza kifungo katika Gereza la King’ang’a- Kondoa.

“Kwenye hati yake ya kumaliza kifungo inaonesha ni mfungwa namba 46/2022 kuanzia Agosti 13 mwaka 2021 hadi Februari 11 mwaka 2022.”

“Anaonekana alikuwa mhalifu mzoefu kwani aliwahi kumjeruhi kichwani dada yake wa tumbo moja kwa panga, na alijiwekea himaya kwa mtu yeyote aliyekuwa akipita katika eneo lake alikuwa akimshambulia kwa mishale,” alisema.

Alisema pia umbali wa takribani mita 200, Sango alichimba mahandaki mawili ambayo huyatumia kujificha mara afanyapo matukio ya uhalifu.

Habari Zifananazo

Back to top button