Auawa kwenye baa yake kwa wivu wa mapenzi

DAR ES SALAAM: JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata mkazi wa Goba Lastanza, Kinondoni, Joseph Sanura (31) kwa tuhuma ya mauaji ya Penina Rwegoshora (28) mkazi wa Goba Center, Kinondoni kwa madai ya wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema tukio hilo lilitokea asubuhi ya Mei 23, mwaka huu eneo la Penina Pub (baa), maeneo ya Goba Center.

Alieleza kuwa uchunguzi wa awali wa polisi unaonesha kulikuwa na mgogoro wa kimahusiano kati ya mtuhumiwa na marehemu kabla ya kushambuliwa kwa panga na Sanura.

Alisema kuwa upelelezi unakamilishwa ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

HabariLEO lilizungumza na mashuhuda wa tukio hilo, ambao wamedai kuwa Penina aliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na mtuhumiwa huku chanzo cha tukio hilo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kwa mujibu wa majirani, walipata taarifa za kuuawa kwa Penina juzi asubuhi kutoka kwa watu mbalimbali kwa njia ya simu. Mmoja wa marafiki wa karibu wa Penina (hakutaja jina lake) alidai kuwa alipata taarifa hizo wakati akiwa amelala baada ya kupigiwa simu na afande aliyemtaja kwa jina moja la Eliya na kumuuliza kama anamfahamu mwanaume aliyemuua Penina.

“Afande aliponiuliza hivyo nikamwambia mbona nilikuwa naye jana hadi usiku ndipo akaniambia Penina amekufa ikabidi niondoke kwenda kwenye eneo la tukio kuhakikisha kama ni kweli,” alisema. Alimuelezea Penina kama dada mpambanaji anayezungumza na watu vizuri na kuwa kila mtu alikuwa akimfanya kama ndugu yake ambaye wameishi naye kwa upendo.

Alieleza kuwa hafahamu sababu ya mpenzi wa Penina kuchukua maamuzi ya kumuua na kusema walikuwa wakiishi nyumba moja na mtuhumiwa huyo.

Kwa upande wake Emmanuel Francis, alidai kuwa huenda sababu ya mtuhumiwa kuamua kutekeleza tukio hilo ni kwa sababu ya wivu wa mapenzi. “Kwa jinsi walivyokuwa wanaishi na mwanaume wake na taarifa nilizozipata kuwa amemuua sikushangaa sana kwa sababu yule mwanaume alikuwa anampenda sana, nafikiri chanzo itakuwa ni wivu wa mapenzi na kutokana na kazi za Penina huenda alichukulia kuwa ana mwanaume mwingine.

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button