HATUA ya serikali kusema inatafakari maombi ya wabunge kugawa majimbo yao, ikiwa ni pamoja na Jimbo la Mbeya Mjini anapotoka Spika Dk Tulia Ackson, imeungwa mkono na mwandishi nguli wa habari nchini Cosmas Makongo na kueleza kuwa kuna haja pia serikali ikatazama vigezo vya Wilaya ya Chato kuwa Mkoa mpya wa kimkakati.
Akijibu Swali la Mbunge wa Viti Maalum Sophia Mwakagenda Bungeni leo Machi 3, 2023, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, amlisema Dk Tulia ni miongoni mwa wabunge waliowasilisha maombi ya kutaka majimbo yao yagawanywe kutokana na ukubwa na idadi ya wananchi.
“Serikali inatafakari maombi hayo na wakati utakapofika vigezo vitazingatiwa,” amesema Naibu Waziri.
Akizungumzia hilo, Makongo amesema suala la kugawa majimbo au mikoa ni muhimu ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kumpongeza Dk Tulia Ackson kwa kupendekeza kugawanya majimbo ya uchaguzi yenye watu wengi, ikiwemo Jimbo la Mbeya Mjini.
“Mhe.Spika Dk Tulia anatakiwa kuungwa mkono na wananchi wapenda maendeleo kwa kutambua umuhimu wa kuongeza wawakilishi wa wananchi ili wapate huduma karibu za kijimbo kwenye maeneo yao, ili kujenga ukaribu wa wananchi na serikali yao itakayowapunguzia mzigo mkubwa wa kufuata huduma umbali mrefu,” alisema Makongo