Aunguzwa mikono, akosa mitihani darasa la saba

MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi Shahende, Kata ya Butobela halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani hapa amejeruhiwa kwa kuunguzwa mikono na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wa taifa.

Taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo, imethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza ukatili huo umefanywa na mama yake mzazi, ambaye alianza kwa kumpiga na fimbo kisha kumuunguza mikono.

Alimtaja mtuhumiwa wa ukatili huo ni Mpipi Emmanuel (31), ambaye tayari anashikiliwa na vyombo vya dola na majeruhi amepelekwa kituo cha afya cha Kata ya Bukoli na anaendelea kupatiwa matibabu.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Shahende, kata ya Butobelea, Ada Michael amesema tukio lilitokea Oktoba 5, 2022 na alipokea taarifa kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Shahende na kuchukua hatua za kisheria.

“Tulifanya utaratibu wa kumfuatilia mzazi aliyefanya ukatili huo, tukabahatika kumkamata, baada ya kumhoji akadai kwamba binti alikuwa ameiba hela, Sh 30,000, ndio akachukua uamuzi huo,” amesema.

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Edith Mpinzile amekiri mwanafunzi huyo ameshindwa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba, ambapo wamefuatilia lakini bado hakuna taarifa za uhakika juu ya chanzo cha tukio hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button