Avamia kanisani, afanya uharibifu

MTU mmoja amevamia na kufanya uharibifu ndani ya kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Geita, hali iliyosababisha sintofahamu kwa waumini wa kanisa hilo mjini Geita.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassalla ametoa taarifa hiyo leo na kueleza mtu huyo alitenda uharifu huo usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26, 2023.

Askofu Kassalla amesema mtu huyo aliingia ndani ya kanisa kwa muda ambao haujulikani kwa kuvunja kioo katika mlango mkuu na kisha kwenda kuharibu kabisa sehemu ya madhabahu.

Advertisement

“Amevunja tabelanakro, amemwaga ekaristi chini, ameharibu kabisa vifaa vyote vya altaleni, na akafanikiwa kuingia sekaristia kuu na amefanya vilevile uharibifu mkubwa kwa kuvunja vifaa mbalimbali vya ibaada.

“Vile vile mfumo wa kamera za ulinzi inaonekana umeharibiwa kabisa, hatujui kama alianza kwa kuharibu mfumo wa kamera za ulinzi au ameanza na uharibifu huo, binafsi mimi nimetaarifiwa ilikuwa saa nane na dakika 13 usiku,” ameeleza.

Askofu Kassalla amebainisha pia vitabu vya ibaada ndani ya kanisa hilo vimeharibiwa ,ambapo baada ya kupokea taarifa hizo juhudi za kumkamata mtu huyo zilifanikiwa na tayari anashikiliwa na jeshi la polisi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Bertha Kombo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza mtuhumiwa amefanya uharibifu huo kwa kutumia jiwe na tayari amekamatwa.

“Huyu mtu inaonekena alikuwa kama mlevi hivi, lakini pia ni kama kuna kukengeuka kwa maadili kwa sababu huyu mtu inaonekana aliwahi kuhudumu kwenye makanisa toka huko Bukoba (mkoani Kagera), alikotokea,” amesema.