Aweso asisitiza ratiba ya mgao wa maji

WAZIRI Maji Juma Aweso ameiwataka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasa) kuzingatia ratiba ya mgao wa maji katika Jiji la Dar es Salaam ili kila mwananchi aweze kupata huduma kulingana na kiwango cha maji kilichopo kwa sasa.
Aweso alitoa kauli hiyo jana alipotembelea eneo la Tandale Dar es Salaam ambapo kazi ya ufukuaji na usafishaji wa visima vilivyochimbwa miaka ya nyuma ili viweze kutumika kwa lengo kuhakikisha wananchi waishio Mkoa wa Dar es Salaam wanapata huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani inaendelea.
“Nimefika hapa Tandale ambapo kuna zoezi la ufukuaji na usafishaji wa visima vilivyochimbwa miaka ya nyuma ili viweze kutumika katika kipindi hiki ambacho kuna upungufu wa maji, lengo ni kuhakikisha wananchi waishio Mkoa wa Dar es Salaam wanaendelea kupata huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani,” alisema Aweso.
Alisema ametoa agizo kwa Dawasa washirikiane na wadau wengine ili kufanikisha kazi ya uzibuaji wa visima kukamilika. Kazi hiyo inatekelezwa na watu wa Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na DDCA na ni endelevu na visima vyote vitasafishwa na maji yatakayopatikana yataunganishwa katika mitambo ya Dawasa ili kuwahudumia wananchi.
Tayari kazi ya kuboresha kisima kingine cha maji eneo la Mwananyamala Komakoma wilayani Kinondoni chenye urefu wa mita 39, imeanza ili kuingiza maji kwenye mfumo wa usambazaji wa Dawasa kwa lengo la kuongeza upatikanaji kwa wakazi wa Mwananyamala.
Kinondoni na Magomeni wanahudumiwa na kisima chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 100,000 kwa saa ni miongoni mwa visima vinavyoboreshwa kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu ili kukabiliana na upungufu wa huduma ya maji.
Tayari serikali imesema kwa sasa hali ya kiwango cha uzalishaji wa maji katika Mto Ruvu kimepungua kwa asilimia 64 kutokana na ukame uliotokana na ukosefu wa mvua za vuli uliosabishwa na mabadaliko ya tabia ya nchi.
Mpaka Oktoba mwaka huu uzalishaji wa maji ulikuwa umeshuka kutoka lita milioni 466 mpaka kufikia lita milioni 300.