Aweso atoa maelekezo maji Wami Sokoine

WIZARA ya Maji imeuagiza Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), kutoa fedha ya dharura Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa uchimbaji kisima kirefu cha maji eneo la Wami Sokoine ( Ranchi ya Wami -Sokoine),Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, ambalo wakazi wa maeneo hayo wanatumia maji yasiyo salama ya kwenye madimbwi.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso alitoa agizo hilo mjini Morogoro kwa uongozi wa mfuko huo wakati wa ziara ya kutembela, kukagua na kuzindua miradi ya maji.
“ Kuna eneo la Ranchi ya Wami Sokoine ukipita kwenda Dodoma kuna watu pale huwa wanahangaika na maji, wanachukua maji kwenye madimbwi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
“Hii hapana , Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametuelekeza sisi Wizara ya Maji jukumu letu mahususi watu wapate maji, “ alisema Aweso.
Kutokana na hali hiyo aliuagiza mfuko huo kutoa fedha ya dharura Sh milioni 100 na kukabidhiwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), kwa ajili ya kazi ya uchimbaji visima virefu iweze kuanza mara moja katika eneo hilo.
Aweso alisema kuwa dhamira ya Rais ni kuona wananchi wa mijini na vijijini wanapata maji safi na salama, hivyo alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa kusimamia jambo hilo ndani ya muda mfupi.
“ Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji na lengo ni kuhakikisha watu wanapata huduma ya maji na sasa tuongeze kasi katika utoaji wa huduma, ili mambo yaende sawa,” alisema Aweso
Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja, alisema kwa jukumu la usimamizi wa utoaji wa huduma za maji eneo hilo lipo chini ya Moruwasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa , Mhandisi Tamim Katakweba alisema baada ya kukabidhiwa usimamizi wa maji eneo hilo, tayari umefanyika upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji na kuwasilisha maombi ya kupata fedha ili kazi ianza mara moja.