AZAM FC huenda ikarejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara endapo leo itapata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi hiyo utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mchezo uliopita Azam FC ilitoa kipigo cha mabao 4-3, dhidi ya Mtibwa Sugar, ushindi ambao uliwaweka kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya juzi kuondolewa na mabingwa watetezi Yanga baada ya kuifunga Kagera Sugar bao 1-0.
Maafande wa Ruvu Shooting wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare na maafande wenzao wa Tanzania Prisons, lakini kabla ya mchezo huo huko nyuma wamepoteza mechi tatu mfululizo, jambo ambalo huenda likaufanya mchezo wa leo kuwa na ushindani.
Katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam FC, haikutumia wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza kutokana na matatizo mbalimbali, ikiwemo kadi za njano na majeraha lakini katika mchezo huo wengi wao wanatarajiwa kuwepo.
Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kally Ongala alisema kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yamekamilika na vijana wake wapo tayari kuyafanyia kazi yale ambayo yeye na wasaidizi wake wamewaelekeza kwenye uwanja wa mazoezi.
Kally ameeleza kuwa lengo lao ni kuendelea kuchukua pointi tatu ili kurudi kileleni na kuwaongezea presha wanaowafukuzia huko nyuma na amewaeleza wachezaji wake umuhimu wa ushindi katika mchezo huo.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa ameeleza kuwa wanajua ugumu wa mchezo huo na ubora wa timu wanayokutana nayo leo, lakini amewaandaa vizuri wachezaji wake kuhakikisha hawapotezi mchezo.
Alisema tangu kumalizika kwa mchezo wao wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons tayari walishaanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa Azam FC, hivyo wapo tayari kwa mapambano na anaamini kuwa leo ndio siku yao ya kuzinduka.