YANGA leo usiku itacheza mchezo wake wa mwisho hatua ya makundi Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida Big Stars, lakini mawazo ya Kocha Msaidizi wa Azam FC Kally Ongalla ni kutaka kukutana na Yanga hatua ya Nusu Fainali.
Kutokana na hali hiyo Ongalla amesema anaiombea Yanga ishinde leo dhidi ya Singida Big Stars na ifuzu Nusu Fainali, kwani yeye anataka kukutana na Yanga, ili kulipa kisasi cha kufungwa na timu hiyo kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Naiombea Yanga ishinde ili nikutane nayo kwenye Nusu Fainali, lengo langu ni kutaka kulipa kisasi unajua nimekutana nao mara mbili kwenye ligi na zote hatukuweza kuwafunga nadhani ikitokea hii itakuwa nafasi nzuri kwetu kulipa kisasi,” amesema Ongala.
Ili ifuzu Nusu Fainali, Yanga italazimika kuifunga Singida Big Stars leo na kuongoza Kundi B.
Timu hizo zitaingia uwanjani huku Singida Big Stars ikiwa inaongoza msimamo wa kundi wakiwa na pointi tatu sawa na Yanga, lakini wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga, ambapo sare ya aina yoyote Singida itakuwa imetinga Nusu Fainali.