AZAM FC imeendelea kuvutwa shati baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Geita Gold FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Nyankumbu Geita jana.
Matokeo hayo yameendelea kuiweka timu hiyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakifikisha pointi 37 sawa na Simba iliyopo nafasi ya pili huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja kabla ya Simba kucheza jana usiku wakati Geita wameshuka hadi nafasi ya sita wakifikisha pointi 23.
Mabao katika mchezo huo, Azam FC ndio walianza kufunga bao dakika ya 15 mfungaji akiwa Prince Dube na Offen Chikola akaisawazishia Geita dakika ya 69 kwa mkwaju wa penalti.
Kipindi cha pili Geita ambao mchezo uliopita walipoteza kwa kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Simba, walionesha uhai na kulishambulia lango la Azam FC lakini walinzi wake walitimiza vyema majukumu yao.
Katika mchezo wa mapema uliochezwa Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya wenyeji Tanzania Prisons waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Ushindi huo umeipandisha Prisons hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wakifikisha pointi 18 huku Dodoma Jiji ikibaki nafasi ya 12 na pointi 18.
Mabao ya washindi katika mchezo huo yamefungwa na Zabona Mayombya dakika ya tatu na bao la pili limefungwa na Samson Mbangula dakika ya 90.