CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa katika mchakato wa kuwa na viongozi wa ngazi mbalimbali tangu ngazi za mashina hadi taifa.
Katika uchaguzi huo, Watanzania wameshuhudia wanachama wakitumia demokrasia yao kuchagua viongozi ambao kwa imani yao, watakivusha chama katika uchaguzi mwingine unaofuata.
Si siri kwamba, mara zote uchaguzi huwagawa watu kiimani kwani wapo wanaoamini mgombea fulani anafaa kuongoza, huku wengine wakiona kinyume hivyo kuwa na makundi yanayotofautiana kimtazamo.
Kutokana na hilo, ndipo makundi yanayoshindana hupiga kampeni ama za waziwazi au za siri mradi tu mgombea wanayemtaka apate ushindi na hapo ndipo pia waungwana huzingatia usemi kuwa asiyekubali kushindwa si mshindani.
Sisi tunawapongeza wote wanaoshiriki kampeni na mchakato mzima wa uchaguzi ndani ya chama hicho tawala kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Aidha, tunawapongeza wote ambao kwa kufuata taratibu zilizopo wameibuka na ushindi na sasa watakiongoza chama kwa nyadhifa na maeneo yao.
Wakati tukitoa pongezi hizo, pia tunazihimiza mamlaka za kichama na kisheria kukaza uzi wa kisheria dhidi ya wote waliofanya ndivyo sivyo katika uchaguzi kwa kuwa hao hawakuwa na nia njema kwa chama na jamii kwa ujumla.
Sisi tunajua kuwa katika harakati hizo za kisiasa ndani ya chama tawala hicho, ni dhahiri kulikuwa na makundi yaliyokuwa ‘yakipambana’ hapa na pale.
Tunasema walioshinda hongera na wale ambao kura hazikutosha wasikate tamaa badala yake wajiandae kwa uchaguzi mwingine ujao huku wakiendelea kukitumikia chama chao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa makundi hayo ambayo kimantiki hayaepukiki, uchaguzi umefanyika, viongozi wamepatikana na sasa ni muda sahihi kuvunja makundi hayo ndani ya chama na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Tunasema hivyo kwa kuwa CCM mbali na kuwa chama kikongwe nchini, ndicho kilichoshika hatamu, hivyo ndicho chama kinachotegemewa kuielekeza serikali kulingana na Ilani ya Uchaguzi.
Ni wakati sasa makundi ndani ya chama yavunjwe ili chama kijiandae kwa uchaguzi mwingine ukiwamo wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Wakati tukisema hayo, tunavihimiza vyama vingine pia kufuata nyayo za kufanya chaguzi kwa amani na utulivu kama kilivyofanya CCM.
Kwamba, waliobainika kufanya ‘ndivyo sivyo’ wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za chama na nchi kwa ujumla.
Ndio maana tunasema baada ya uchaguzi huu wa ndani, wanachama wa CCM ambacho ni chama tawala, waendeleze umoja katika kukitumikia chama chao na taifa kwa ujumla ili kiwe kioo kwa vyama vingine.