KIKUNDI cha sanaa mkoani Arusha, Baba Afrika Entertainment kimeeleza kuja na mikakati mipya kwa ajili ya kuifikia jamii kwa wingi na kuielimisha kupitia sanaa.
Baba Afrika Entertainment kinajihusisha na sanaa ya maigizo kufikisha ujumbe mbalimbali katika jamii kupitia maigizo.
AKizungumza jijini hapa kiongozi wa kikundi hicho Masanja Pius ‘ baba Afrika ‘ ameeleza kuwa wanajihusisha na Sanaa za jukwaani ‘sanaa faraguzi’ hususani kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo afya, Elimu na kupinga ukatili.
“Tumekuwa tukifika maeneo mbalimbali na kwa mwaka huu tumetumia Sanaa yetu kwenda mashuleni kuelimisha,kuburudisha na kuwapatia njia sahihi zinazofaa kupitia na kujifunza mambo yaliyo sahihi ” amesema Pius.
Amesema mwaka ujao wamejipanga kufika maeneo mbalimbali si tu kutoa burudani bali kutoa elimu kwani jamii nyingi na kwa sasa walizozifikia zimekuwa na matokeo chanya na uelewa umeongezeka katika masuala mbalimbali.
” Hivi karibuni tulifika wilayani Longido, Arusha ambapo tulikutana na vijana ambao tuliwasisitiza na kuwapatia elimu kutambua umuhimu wa vituo vya afya katika kupima afya zao pia tulitoa elimu kupitia sanaa ya maigizo kupinga ukatili kwa wanawake na watoto ikiwa na pamoja na ndoa za utotoni na kwa sasa tunalenga kuifikia jamii kwa wingi zaidi. ” amesema Pius.
Amefafanua kuwa watawatafuta wadau ili wazitambue kazi zao pamoja na kuvishirikisha vyombo vya habari kwani elimu ya Sanaa ni njia mojawapo katika kutatua matatizo mbalimbali.
Ameongeza kuwa kwa sasa matokeo ni makubwa kwani wamekuwa wakifanya kazi na Serikali katika matukio mbalimbali pia wadau na wote kuwa wamekuwa wakitambua na kuona umuhimu wa kufikisha ujumbe kupitia Sanaa.
Kikundi cha Sanaa cha Baba Afrika Entertainment kilianza rasmi mwaka 2010