Baba aua, amfukia porini mtoto mlemavu

Baba aua, amfukia porini mtoto mlemavu

JESHI la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Elias Bakumye (32),  mkazi wa Kijiji cha Chikobe, Kata ya Butundwe Wilaya ya Geita kwa tuhuma za kumuua mwanaye mlemavu wa viungo na kumzika porini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha tukio hilo leo na kueleza mtoto alikuwa na umri wa miaka mitano na mwili uliokotwa na wasamaria wema Aprili 12, 2023  majira ya saa tatu asubuhi.

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo walituma timu ya upelelezi kwenda kijijini eneo la tukio, ambapo baada ya kufika kule kweli ule mwili ulikutwa na kuonekana yule marehemu alikuwa mlemavu.

Advertisement

Amesema baada ya taarifa kusambaa uchunguzi ulifanyika na hatimaye mzazi wa mtoto alipatikana, ambapo alihojiwa na kukiri kumuua mtoto huyo kwa madai kwamba alishindwa malezi ya yule mtoto.

“Walitalakiana na mke wake ambaye amerudi kwao, lakini baada ya mke kurudi kwao alimwachia mtoto huyo wa miaka mitano, ambaye ni mlemavu anayehitaji huduma zote.

RPC wa Geita, Safia Jongo

“Akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja akaona hawezi kuendelea kumuhudumia yule mtoto, akaamua kumbeba yule mtoto kumpeleka kwa mama yake ambaye alikuwa anaishi kwa wazazi wake.

“Alivyofika kule wazazi pamoja na yule mwanamke mtalaka wake, wakakataa kumpokea yule mtoto, wakamwambia arudi naye kwani yeye ndio baba mzazi.

“Alipofika eneo la porini hapo anakiri kwamba akaona hataweza kumuuguza huyu mtoto, kwa hiyo akambana pumzi na kumuua na hatimaye akamfukia, lakini hakumfukia vizuri, ” amefafanua Kamanda.