DODOMA: WIZARA ya Afya, imewataka Watanzania kuazimia kulinda na kutunza afya zao hususani katika nyakati hizi za Sikukuu za mwisho wa mwaka na mwaka mpya 2024.
Akiwasilisha ujumbe huo kwa umma, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kujali afya zao, kwani kujisahau ni kukaribisha magonjwa hatari ikiwemo yale yasiyoambukiza.
“Ewe Mtanzania mwenzangu, weka azimio la kulinda na kutunza afya yako, badili mtindo wa maisha, kula chakula bora na fanya mazoezi angalau mara tano kwa wiki,” amesema waziri huyo
Kupitia kampeni ya ‘Mtu Ni Afya’, kiongozi huyo amesema ni muhimu kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya, ikiwemo kuepeka na msongo wa mawazo.
Lishe bora maana yake ni kula chakula cha kutosha chenye virutubisho vyote muhimu. Lishe bora husaidia mwili kukua vyema, kuujenga mwili lakini pia huimarisha kinga ya mwili ili kuweza kupigana na magonjwa.
Ili lishe iwe bora ni muhimu iwe na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali kama vile protini, wanga, fati, mbogamboga, madini, matunda na maji kwa wingi.