Bajaji za katikati ya jiji kuwekwa alama

DSM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Edward Mpogolo amesema serikali inaandaa utaratibu wa vyombo vyote vya moto zikiwemo bajaji zitakavyoingia katikati ya jiji kuwekewa alama na namba za utambuzi sambamba na kuwekewa maegesho.

Mpogolo alisema hayo mwishoni mwa wiki alipofanya mkutano wake na Umoja wa Walemavu Waendesha Bajaji Dar es Salaam (Uwawada) waliotoa changamoto zao kwa kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), Hamad Komboza alitaja changamoto zinazowakabili wenye ulemavu wanaoendesha vyombo vya moto.

Alisema baadhi ni kuchanganyika na wasio na ulemavu wanapoingia katikati ya mji, hali inayowasababisha kukosa abiria kwani wao hawawezi kushindana na wazima, huku changamoto nyingine ikielezwa kuwa ni maegesho ya bajaji ya pamoja.

Baada ya kusikiliza changamoto hizo, Mpogolo aliutaka umoja huo kuwa na utulivu na kuwahakikishia serikali itazitatua changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa utaratibu wa vyombo vyote vitakavyoingia katikati ya jiji kuwekewa alama na namba za utambuzi.

Lakini pia, alisema serikali inaendelea kushughulikia changamoto za maeneo ya maegesho, mwingiliano na watu wasio na ulemavu pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa kundi hilo maalumu.

Alisema uamuzi huo unatokana na kikao cha kamati ya usalama barabarani, baada ya kukubaliana juu ya jambo hilo na kusisitiza suala hilo linasubiri baraka za vikao vingine na kisha kuundiwa sheria ndogo ili liweze kutekelezeka.

“Tunaweka alama na namba ili yeyote atakayeingia katikati ya mji mtajua huyu si mwenzenu..hivyo niwaombe mnapokuwa mnajadili na kuazimia wekeni na utaratibu wa nini kifanyike kwa atakayekwenda kinyume na maazimio yenu,” alisema Mpogolo

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button