Bajeti Iringa yaongezeka kwa Sh Bil 3

Bajeti Iringa yaongezeka kwa Sh Bil 3

BAJETI ya mapato na matumizi ya halmashauri ya wilaya ya Iringa kwa mwaka wa fedha ujao wa 2023/2024, inatarajia kuongezeka kwa zaidi ya Sh Bilioni tatu.

Akiwasilisha rasimu ya mpango wa bajeti hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani, Ofisa Mipango wa halmashauri hiyo, Exavery Luyangaza alisema katika mwaka huo wa fedha wanategemea kukusanya na kutumia zaidi ya Sh Bilioni 60.2.

Alisema ongezeko hilo ni kutoka bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 ya zaidi ya Sh Bilioni 57.3.

Advertisement

“Mapato na matumizi hayo ni kutoka bajeti ya Serikali Kuu na vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani vya halmashauri yetu,” alisema.

Akizungumzia mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha, Luyangaza alisema hali ni ya kutia moyo kwani yameongezeka kwa asilimia 17 kutoka asilimia 15 walizokuwa wamepangiwa.

“Mapato yameongezeka kwa zaidi ya Sh Milioni 700 kutoka zaidi ya Sh Bilioni 4.2, zilizotarajiwa kukusanywa hadi zaidi ya Sh Bilioni 4.9. Haya ni mafanikio makubwa katika kusaidia utekelezaji wa majukumu ya halmashauri,” alisema.

Likikubali na kuupitisha mpango huo wa bajeti ya Mapato na Matumizi wa zaidi ya Sh Bilioni 60.2 katika kikao chake maalumu leo mjini Iringa, baraza la madiwani la halmashauri hiyo limewataka wataalamu wake kuendelea kuboresha na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

“Boresheni vyanzo vya mapato vilivyopo ili kuimarisha mkakati wa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na serikali kuu, lakini pia endeleeni kubuni vyanzo vipya endelevu ili kuwezesha utekelezaji wa mpango huu wa bajeti tulioupitisha,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa.

“Ninawapongeza wataalamu wa ngazi zote, ofisi ya mkuu wa wilaya waheshimiwa madiwani na wadau wote wa maendeleo kwa ushirikiano wao unaowezesha kusukuma gurudumu la maendeleo la halmashauri yetu licha ya changamoto zilizopo,” alisema bila kuzitaja changamoto hizo.

Mhapa ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa Dk Samia Suluhu Hassan, akisema imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni  pamoja na ya maji, barabara, umeme, elimu na afya miradi ambayo kama ingekuwa inatakiwa kutekelezwa kwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, kazi hiyo isingeweza kufanikiwa.

Kwa kupitia mpango wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha Mhapa aliitaka halmashauri yake kujikita katika kutekeleza shughuli zinazolenga kutekeleza mikakati ya kukuza uchumi wa halmashauri na watu wake.

Kwa upande mwingine, madiwani wa halmashauri hiyo wamewapongeza wataalamu kwa uandaaji mzuri wa bajeti hiyo na kuwahakikishia wananchi wao kwamba ina mambo mengi mazuri kwa maendeleo yao.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *