BAADA ya Juni 15, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kusoma bungeni taarifa ya Hali ya Uchumi 2022 na Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24, wiki hii wabunge watajikita kujadili hali ya uchumi na bajeti hiyo.
Dk Mwigulu alitoa hoja Bunge lijadili na kupitisha Makisio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Sh trilioni 44.39, kati yake Sh trilioni 30.310 ni za matumizi ya kawaida na Sh trilioni 14.
08 ni kwa ajili ya maendeleo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya serikali kuu na serikali za mitaa.
Katika kuwasilisha bajeti hiyo, Dk Mwigulu alipendekeza kurekebisha, kuanzisha, kufuta na kuongeza ada na tozo zinazotozwa na wizara, idara, taasisi zinazojitegemea ili kuleta usimamizi bora wa sekta mbalimbali na kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Kutokana na wasilisho hilo, kwa wiki nzima kuanzia leo wabunge watachambua bajeti hiyo ambayo pamoja na mambo mengine imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa wananchi na kuanzisha mpya.
Baadhi ya tozo zilizoondolewa ni za laini za simu, kuondolewa ada za vyuo vya ufundi, kuondolewa ada ya leseni za hati.
Tozo zilizoongezwa ni pamoja na ushuru wa magari, saruji pamoja na umiliki wa silaha mbalimbali.
Baadhi ya kodi zilizoanzishwa ni pamoja na bodaboda na bajaji kuanza kulipa kodi, matangazo ya mitandaoni nayo yatakuwa yakilipiwa kodi.
Lakini waziri pia alipendekeza kupigwa marufuku kufungwa biashara kwa kosa la kodi na tozo za mizigo bandarini.
Miongoni mwa ada za leseni zilizopungua ni za biashara ya huduma za malazi kwa zile zinazomilikiwa na Watanzania kutoka Dola za Marekani 2,000 hadi 1,500 kwa hoteli ya nyota tano wakati tozo za malazi kwa hoteli ya nyota moja zimeshuka kutoka Dola za Marekani 1,000 hadi Dola za Marekani 200.
Waziri wa Fedha pia alipendekeza kuanzisha utaratibu wa kutoa vibali vya uagizaji wa mafuta ghafi ya kupikia baada ya kupata uthibitisho wa uzalishaji na uchakataji wa bidhaa bakaa.
Wabunge kwa wiki nzima watakuwa na nafasi ya ama ya kuunga mkono mapendekezo ya serikali, kurekebisha au kushauri kufuta baadhi ya tozo na ada pamoja na kodi kadiri watakavyoona inafaa kwa mustakabali wa nchi.
Ikumbukwe kwamba wakati Bunge la Tanzania likijadili bajeti hiyo pia wabunge wa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa wakijadili bajeti za nchi zao ambazo zote ziliwasilishwa wiki iliyopita.
Wiki hii, itahitimishwa kwa mijadala tu hadi Juni 27, mwaka huu ambapo mijadala itahitimishwa kwa wabunge kuitwa majina na kupiga kura kupitisha bajeti hiyo. Mkutano wa Bajeti ulionza Aprili 4 utaahirishwa Juni 30, mwaka huu.