Bajeti ya kilimo yazidi kupaa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024, serikali itaongeza bajeti ya sekta ya kilimo hadi kufi kia zaidi ya Sh trilioni moja.

Aliihakikishia jumuiya ya kimataifa kwamba serikali ya Tanzania itaendelea kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuifanya nchi kuwa ghala la chakula duniani.

“Mwaka ujao wa fedha tutaongeza tena bajeti hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni moja na kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo ambayo tunaamini itaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuishirikisha sehemu kubwa ya jamii wakiwemo vijana ambao kupitia Programu ya BBT (Build Better Tomorrow), iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imelenga kuwakusanya vijana na kuwapatia ujuzi wa masuala ya kilimo,” alisema Dk Mwigulu.

Alitoa kauli hiyo wakati aliposhiriki mdahalo wa viongozi wa ngazi ya juu wa nchi za Afrika kuhusu chakula na kilimo ulioandaliwa na Taasisi inayojihusisha na Uhamasishaji wa Masuala ya Kilimo Afrika (AGRA). Dk Mwigulu yuko nchini Marekani kuhudhuria mikutano ya kipupwe iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika Washington D.C.

Alisema serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka wastani wa Sh bilioni 250 hadi kufikia Sh bilioni 950 katika bajeti inayotekelezwa hivi sasa na kwamba mwaka ujao, bajeti hiyo itaongezwa ili kutimiza malengo ya serikali ya kuifanya sekta hiyo kuwa na tija.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo Tanzania iliyoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, Frank Nyabundege alisema benki hiyo imewekeza zaidi ya Sh bilioni 500 katika kuendeleza kilimo Tanzania kwa kuwawezesha wakulima wa kati, wakubwa pamoja na taasisi kadhaa zinazojihusisha na kilimo. Nyabundege alisema juhudi hizo zitaendelezwa kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGRA, Hailemariam Dessalegn aliisifu Tanzania kwa mikakati inayoichukua ya kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuwahusisha vijana na kwamba mpango huo unatakiwa kuigwa na nchi nyingine barani Afrika.

Dessalegn ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia, alisema usalama wa upatikanaji wa chakula cha kutosha pamoja na usalama wa chakula, vinahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha na kwamba mfano unaotolewa na Tanzania katika kusukuma mbele ajenda ya nchi kujitosheleza kwa chakula, ni muhimu na kuahidi kuwa AGRA itaendelea kusaidia juhudi hizo.

Mkuu wa Idara ya Utawala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani, Isobel Coleman alisema taasisi yake imejitahidi kuwekeza fedha katika nchi mbalimbali duniani kuendeleza kilimo pamoja na usalama wa chakula kwa kuwa ajenda ya kilimo endelevu na cha uhakika ni muhimu kwa ustawi wa wananchi wakiwamo watoto.

Katika mdahalo huo, nchi za Kiafrika ziliombwa kuweka utashi wa kisiasa kwa kuhakikisha kilimo kinapewa kipaumbele kwenye mipango yao ya kitaifa kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kutoka asilimia 10 za sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, utafiti na maofisa ugani.

Pia kuwa na masoko ya uhakika, kuwashawishi vijana kushiriki shughuli za kilimo, kuongeza mauzo nje ya nchi kutoka Dola za Marekani milioni 750 hadi kufikia dola bilioni mbili kwa mwaka ili kukuza uchumi na maisha ya watu kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button