Bajeti ya tril 49/- kuleta nafuu

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba

SERIKALI inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 49.35, sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/2024.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya serikali kwa mwaka 2024/2025 jana bungeni.

Alisema ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharimia deni la serikali lililoongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani, ajira mpya na ulipaji wa hati za madai.

Advertisement

Pia ni bajeti kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na maandalizi ya Michuano ya mpira wa miguu ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwamo ujenzi na ukarabati wa viwanja.

Dk Mwigulu alisema mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa Sh trilioni 34.61 sawa na asilimia 70.1 ya bajeti yote na asilimia 15.7 ya Pato la Taifa.

Alisema mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuwa Sh trilioni 29.41, mapato yasiyo ya kodi yatakayokusanywa na wizara, taasisi na idara zinazojitegemea Sh trilioni 3.84 na mapato yatakayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Sh trilioni 1.36.

Pia misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inakadiriwa kuwa Sh trilioni 5.13.

Dk Mwigulu alisema serikali inakadiria kukopa Sh trilioni 6.62 kutoka soko la ndani.

Sh trilioni 4.02 ni kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za serikali zinazoiva na Sh trilioni 2.6 kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo. Alisema pia serikali inakadiria kukopa Sh trilioni 2.99 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.

Matumizi

Dk Mwigulu alisema serikali imepanga kutumia Sh trilioni 49.35, kiasi kinachojumuisha Sh trilioni 15.74 kwa ajili ya ulipaji wa deni la serikali na gharama nyingine za mfuko mkuu na Sh trilioni 11.77 kwa ajili ya mishahara ikiwamo ajira mpya pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi.

Pia Sh trilioni 2.17 ni kwa ajili ya mifuko ya reli, barabara, maji, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) na ruzuku ya maendeleo ya Sh trilioni 1.19 kwa ajili ya kugharimia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati pamoja na Programu ya Elimu Msingi na Sekondari bila ada.

Mwigulu alisema dhima kuu ya bajeti ni mageuzi endelevu ya kiuchumi kupitia uimarishaji wa sera za kibajeti, uwekezaji katika kuhimili, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa maendeleo ya wananchi. Alisema shabaha za uchumi ni kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023.

SOMA: Wadau wasifia bajeti kugusa wananchi

Pia ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei. Bajeti nafuu Miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa na waziri ni ya uboreshaji wa mfumo wa kodi, ada na tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mwigulu alisema kuna mazingira yasiyo na usawa yaliyozoeleka katika utozaji wa kodi akitoa mfano wa mtu mwenye kima cha chini cha mshahara anayepata Sh 300,000 kwa mwezi anayetozwa kodi sawa na ilivyo kwa mfanyabiashara mdogo mwenye mapato ghafi yanayozidi Sh 330,000 kwa mwezi.

“Hii haipo sawa na haina usawa. Kwa mfano, mtu mwenye ng’ombe 9,000 kutokulipa kodi na kutaka kujengewa josho au bwawa kwa ajili ya mifugo yake kwa kodi ya mtu mwenye kipato cha shilingi 300,000 kwa mwezi, si sawa,” alisema Dk Mwigulu.

Aliongeza, “mtu mwenye kipato cha shilingi milioni 200 au 300 kutokana na kuuza mazao yake kutokulipa kodi na kupokea ruzuku ya mbolea, mbegu au skimu ya umwagiliaji kutokana na kodi ya mtu mwenye kipato cha shilingi 300,000, sio sawa.”

Kwa mujibu wa waziri, uboreshaji huo unatarajiwa kukidhi kiu ya jamii ya Watanzania katika kuchachua uwekezaji kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ndani ya nchi.

Pia utawekwa mkazo katika sekta za kimkakati kama vile viwanda, kilimo, madini, utalii, ufugaji na uvuvi, miundombinu ya umeme, uchukuzi na usafirishaji na sekta za kijamii za elimu na afya.

Serikali imependekeza msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuchochea uzalishaji.

Amependekeza pia kufuta msamaha wa kodi hiyo kwenye madini ya thamani, madini ya vito na madini mengine ya thamani yanayouzwa kwenye vituo vya kusafishia dhahabu vilivyopo nchini.

Mapendekezo mengine ni kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye mbolea inayozalishwa ndani ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa lengo la kuleta nafuu kwa wakulima na walaji.

Nafuu nyingine inatarajiwa kutokana na mapendekezo ya kusamehe VAT kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja ili kuendeleza unafuu wa bei ya mafuta ya kula iliyopanda kutokana na mdororo wa uchumi pamoja na vita ya Urusi na Ukraine.

Ushiriki sekta binafsi Dk Mwigulu alisema misingi ya bajeti ni kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara na kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwamo ukame, vita, magonjwa ya mlipuko na mafuriko.

Vipaumbele

Dk Mwigulu alisema bajeti imelenga kutekeleza vipaumbele vya kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.