KATIBU Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Mruma amewataka waumini wa dini ya Kiislamu nchini na Watanzania kwa ujumla kujitokeza na kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika nchi nzima Agosti 23.
Aidha, amewahimiza viongozi pamoja na waumini wa dini hiyo, kuitumia ibada ya Ijumaa hii ya mwisho kabla ya siku ya sensa kufanya dua maalumu ili kulikabidhi jambo hilo kwa Mungu na liwe na mafanikio hasa baada ya kufanyika kazi kubwa ya uhamasishaji, suala litakalotolewa tamko na viongozi wa juu wa dini hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mruma alisema sensa ni jambo la taifa linalohusu maendeleo ya wananchi wote pasipo kujali imani za kidini, kabila, mila wala desturi hivyo ni muhimu kila mtu akashiriki kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
“Nawaomba wananchi wote kuhakikisha tunaitumia siku ya Agosti 23 kushiriki kikamilifu katika sensa ili kusaidia kufanikisha malengo ya taifa letu katika kujiletea maendeleo,” alisema.
Aidha, amewaagiza viongozi wa misikiti yote nchini pamoja na sehemu zingine za ibada kutumia fursa na nafasi zao kuhamasisha waumini wao kujitokeza kushiriki mchakato huo ili kuiwezesha serikali kuwa katika nafasi nzuri ya kutoa huduma bora na sahihi kwa wananchi wake.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha analiletea taifa maendeleo hivyo hata hatua yake ya kutaka sensa ifanyike amelenga kufahamu idadi ya wananchi wake ili aweke mipango mizuri zaidi