MUFTI wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ali ametimiza miaka minane ya kuongoza Waislamu huku akijivunia maendeleo aliyofanikisha yakiwemo ujenzi wa zahanati 120 katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kuwaunganisha Waislamu kuwa kitu kimoja.
Kiongozi huyo ambaye ndiye Shehe Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) alisema hayo jana wilayani Kinondoni, Dar es Salaam wakati wa kumbukumbu ya miaka minane ya uongozi wake ndani ya Bakwata tangu 2015.
Alisema wakati akichukua uongozi wa chombo hicho mambo mengi hayakuwa sawa ikiwemo mpasuko ndani kwa Waislamu ambapo walikuwepo wanaopinga na kuunga mkono chombo hicho na kuongeza kuwa kwa sasa Waislamu wote wamekuwa kitu kimoja na wanajivunia kujitambulisha kupitia Bakwata.
Mufti aliongeza kuwa baada ya kuingia madarakani aliamua kubadili mfumo wa kuchagua viongozi wa Bakwata mikoani na wilayani kwa sababu mfumo wa kupiga kura ulikuwa na uwezo wa kutoa viongozi wasiofaa ambapo alibadili mfumo na sasa viongozi hao wanachaguliwa kupitia Baraza la Ulamaa.
“Kwa sasa tunajenga zahanati 120 nchi nzima kwa sababu tumeamua kuifanya Bakwata kuwa chombo cha huduma za kijamii.
“Tunajenga vyuo vya mafunzo ya dini kila mkoa na wilaya na nitumie fursa hii kuwataka mashehe wa mikoa na wilaya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa wale ambao bado,” alisema.
Alisema Bakwata imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondoa uhasama baina ya Waislamu nchini tangu aingie uongozini miaka minane iliyopita na sasa Waislamu wanaigombea kila mtu anataka kuwa kiongozi wa Bakwata.
Mwenyekiti wa Tume ya Maboresho inayoratibu mali za Bakwata ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Wadhamini Bakwata, Suleiman Kova alisema bado kuna watu wanataka Waislamu waendelee kuwa na migogoro kupitia mali za Waislamu na kusema tume yake itashughulika na watu hao kwa kuwa mufti amemuagiza atende haki.
“Endapo mashehe wa mikoa, wilaya na Waislamu kwa ujumla unamjua mtu anayeleta matatizo kuhusu mali za Waislamu, toa taarifa kwangu,” alisema Kova.