Balete: Vijana wa Afrika wana vipato duni
MKURUGENZI Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete, amesema asilimia 70 ya vijana wa kiafrika wanafanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi na yenye kipato kidogo.
Ameyasema hayo leo Mei 19, 2023 kwenye uzinduzi wa maandalizi ya mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika, kuhusu maendeleo ya rasiliamli watu utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 25 hadi 26 mwaka huu.
Amesema, nchi za Afrika zinapaswa kufanya kazi zaidi changamoto ya rasilimali watu inayowakabili japo kuna jitihada kwa serikali zake kuhakikisha watoto wanakwenda shule, tatizo la ajira kwa vijana linapatiwa ufumbuzi na kuhimiza usawa wa kijinsia.
“Tanzania inafanya vizuri ikiwemo kuongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa shule, kuongezeka kwa idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika lakini pia kuna programu za kuwawezesha wanawake.”Amesema na kuongeza
“Nchi za Afrika zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana na wadau zikiwemo asasi za kiraai, sekta binafsi na vijana wenyewe kwa maendeleo ya nchi zao,”amesema Belete