Balozi Amina: Sigombei tena urais
MWANASIASA mkongwe visiwani Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amesema hana mpango wa kuendelea kutia nia ya kugombea urais kwani Rais Samia Suluhu Hassan anatosha.
Mwanasiasa huyo aliyezaliwa Unguja Oktoba 24, 1957, alichukua fomu ya urais wa Zanzibar mwaka 2000 na mwaka 2015 fomu za kuomba kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Balozi Amina anasema aliomba kugombea urais ili kuvunja mfumo wa kuwa na marais wa jinsi moja. “Mimi niligombea urais wa Zanzibar, akateuliwa Karume (Amani Abeid). Michakato yote ilikuwa migumu,” anasema Balozi Amina. Aliongeza: “Sigombei tena, sasa yupo mama (Rais Samia Suluhu Hassan). Anafanya kazi vizuri. Tunamuunga mkono.
Tunasifu kazi yake inaonekana,” alisema wakati anazungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa magazeti ya HabariLEO na Daily News yaliyofanyika nyumbani kwake Mbweni, Unguja.
Balozi Amina anasifu hatua za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha uchumi na maendeleo ya nchi vinafika hadi ngazi ya chini.
Anatoa mfano wa ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, zahanati na madarasa ya kisasa kwa kutumia fedha za Covid-19 na akasema hivyo ni miongoni mwa vitu vinavyoonekana. Aidha, anamsifu Rais Samia na mtangulizi wake, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwa ufuatiliaji kwa wateule na watendaji wengine na kuhakikisha kunakuwa ma utendaji wenye tija serikalini.
“Nashukuru Mzee Magufuli ambaye kwa sasa ni marehemu. Mama Samia na mawaziri naona wanakwenda mbio kabisa. Yeye mwenyewe Rais Samia anahakikisha kwamba anachokisema kinakuwa,” anasema Balozi Amina.
Mwanasiasa huyo anasema mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 haukuwa mwepesi kwake. Anasema msukumo wa kugombea urais ulikuwa ni kutaka nchi ipate Rais mwanamke baada ya kuongozwa na wanaume katika awamu zote kuanza awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, awamu ya nne, Jakaya Kikwete na awamu ya tano, Dk Magufuli.
Balozi Amina anasema miongoni mwa yaliyokuwa magumu katika mchakato huo ni kanuni ambazo jamii ilikuwa imejiwekea kuwa haukuwa wakati wa mwanamke kugombea urais wa Tanzania. “Mojawapo ya principle (kanuni) ambayo nilikutana nayo ni ile kwamba huu si wakati wa mwanamke.
Lakini pia watu walikuwa hawaamini kwamba itakuwaje mtoto wa kike kutoka Zanzibar aje kugombea urais. Niliulizwa maswali,” anasema.
Akizungumzia urais wa Jamhuri ya Muungano, anasema ilimlazimu kutembea mikoa yote kutafuta wadhamini jambo ambalo ilimlazimu kuwa na fedha na watu. “Unatakiwa uwe na fedha au uwe na marafiki wa kukuwezesha, kama huna mtu wa kukupitisha huko huwezi. Kwa hiyo kuna changamoto nyingi,” anasema Balozi Amina.
Anataja jambo lingine aliloliona ni kambi za uchaguzi. “Uchaguzi wa Tanzania ukifika, tunajitahidi zisiwepo kambi lakini tunajidanganya. Kambi zipo,” anasema na kushauri uchaguzi unapomalizika, pia nazo ziishe. Balozi Amina anasema inatakiwa kufahamika kwamba uchaguzi unapoisha, walioshindwa pia wanapaswa kupewa heshima.
“Wameondoka, kura hazikutimia, wanahitaji heshima…lakini kutokana na kuwapo kambi kunakuwa na hofu. Kama tungelikuwa tunafanya kama nchi nyingine, uchaguzi umekwisha, wale walioshiriki uchaguzi wanaheshimiwa, wanapata heshima yao kambi huwa zinavunjika,” anasema.
Akielezea mambo mengine aliyokumbana nayo wakati wa mchakato wa uchaguzi, anasema watu walikuwa hawaamini kuwa amedhamiria.
“Wanaandika kwenye magazeti wanasema muongo huyo. Anajaribu. Hayuko serious (hakudhamiria). Nikawajibu nikasema hapana, kwa sababu naona viongozi wengine tumeingia siku moja serikalini…mimi ndo naonekana siko serious wale wengine ndio waonekane serious,” anasema Balozi Amina.
Hata hivyo, anasema kugombea lilikuwa jambo zuri kwa sababu lilimpa nafasi ya kuona ndani ya CCM kulivyo na pia ilimpa nafasi ya kuona uchumi wa Tanzania kwa kuwa alikwenda mikoa yote. Anataja athari ya uchaguzi kwa mgombea yeyote akisema kunakuwa na maneno na wasiwasi.
“Mpaka ilinichukua kipindi fulani nikapata presha… Lakini nimezaliwa na siasa,” anasema Balozi Amina. Akizungumzia maisha ya kisiasa baada ya uchaguzi, Balozi Amina anakemea kuendelea kwa kambi na akasema walioshinda au kushindwa wanapaswa kuthaminiana.
“Nafikiri pande zote, walioshinda wasiwanyanyapae wale ambao hawakushinda. Wanatengwa… hilo lipo. Unaweza usilione hapo juu lakini ukienda chini unaona inavyokwenda hasa kwa Zanzibar,” anasema. Anasema walioshinda nao wanatakiwa wawashike mkono walioshindwa ili waende sambamba vinginevyo msuguano unaweza kuendelea hadi kwenye uchaguzi mwingine.
“Wawavute, wakae nao, wawape nafasi ili na wao wawe sehemu ya ile serikali ili nao watoe mchango wao kwa sababu wengi wanaoingia ni wale ambao ni wazuri, wana mawazo mazuri, wana uzalendo wa hali ya juu. Na yale makundi yavunjwe,” anasema mwanasiasa huyo.
Balozi Amina anasema pia walioshindwa hawapaswi kukasirika na kuanza kupambana na walioshinda. “Nanyi mlioshindwa, mshirikiane nao kwa moyo mkunjufu. Kama kuna makosa, mnawaambia,” anasema na kuongeza: “Wanaokosolewa, wachukulie ukosoaji katika hali chanya.
” Katika mchakato ndani ya CCM mwaka 2015 kumpata mgombea urais wa Tanzania, Balozi Amina aliingia tano bora akiwa pamoja na wagombea wengine ambao ni Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Bernard Membe (marehemu).
Baadaye aliingia tatu bora kwa ajili ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa chama uliomchagua Dk Magufuli. Balozi Amina sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu Zanzibar