Balozi apigilia msumari ujenzi bomba la mafuta

BALOZI wa Ubelgiji, Luxembourg na Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga ameendelea kukazia kuhusu msimamo wa serikali kuwa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakalosafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, utaendelea kama kawaida.

Amesema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani ni nchi huru haiwezi kuidhinishiwa utekelezaji wa miradi yake na chombo cha nchi nyingine.

Balozi Nyamanga aliyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jana kwa njia ya mtandao wa Zoom ulioratibiwa na Taasisi ya Watch Tanzania.

Alisema bomba hilo litaendelea kujengwa na ndio msimamo ambao serikali imeueleza kupitia Waziri wa Nishati, January Makamba pamoja na nchi ya Uganda.

“Bomba litajengwa kwa sababu Tanzania ni nchi huru na miradi yetu tunayoifanya hatutegemei Bunge la nchi yoyote lituidhinishie ndio tufanye. Sisi ni nchi huru tuna marafiki wengi, lakini hawana mamlaka ya kutuidhinishia nini cha kufanya,” alisema Balozi Nyamanga.

Alisema EU ina taasisi nyingi zikiwemo Kamisheni na Bunge na msimamo uliotolewa na Bunge la umoja huo haumaanishi taasisi zote za umoja huo zina mtazamo huo.

Alisema kuna baadhi ya mambo yamekuwa yakizungumzwa kuhusu bomba hilo, yanayopotoshwa ikiwamo suala la waliohamishwa kwenye mradi kutokulipwa fidia jambo ambalo si kweli.

Alisema kwa upande wa Tanzania wapo waliopisha ujenzi wa bomba hilo walioomba wajengewe nyumba, wengine walitaka walipwe fedha na kwa wale wanaojengewa nyumba mpaka sasa nyumba 37 zimekamilika na 55 ziko kwenye ujenzi.

“Tunachoendelea kufanya kwa jointly (kwa pamoja) tunaendelea kutoa maelezo ya facts ili kuondoa upotoshaji wowote kuhusu huu mradi.

“Tumekubaliana na taasisi nyingine kuwaonesha kutoridhishwa kwetu na kuwaelewesha. Tunataka tuwe na majadiliano ya kisiasa Novemba. Tutaendelea kutoa elimu kuondoa upotoshaji wowote unaoelezwa kuhusu mradi huo,” alisema Balozi Nyamanga.

Alisema Tanzania na EU zina mahusiano na kilichotokea kuhusu Azimio la Bunge la Ulaya ni mazuri na hili lililotokea la azimio la Bunge ni bahati mbaya ambayo imechochewa na baadhi ya maslahi ya kibiashara na kuna upotoshwaji wa mambo mengi.

Alisema Tanzania ilishatoa tamko kwamba nchi iko huru na inatekeleza kwa kuzingatia haki za binadamu.

Bomba hilo la mafuta lenye urefu wa kilometa 1,443, linatajwa kuwa refu zaidi duniani.

Azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya Alhamisi iliyopita lilielezea wasiwasi juu ya haki za binadamu Uganda na Tanzania, unaohusishwa na mradi huo wa uwekezaji katika uchimbaji na usafirishaji wa mafuta.

Shirika la Taifa la Mafuta la China na Kampuni ya Nishati ya Ufaransa ya Total Energies, sambamba na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda na Kampuni ya Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), zimeendelea kusimama kidete katika kuendeleza mradi wa bomba hilo linalotarajiwa kuanza kusafirisha mafuta mwaka 2025.

Hivi karibuni, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliapa kuendelea na mradi huo na kupuuza Azimio la Bunge la EU lililotaka mradi huo uahirishwe kwa tuhuma kuwa unakiuka haki za binadamu.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button