Balozi: Bomba la mafuta ni shukrani kwa Tanzania

BALOZI wa Uganda nchini, Fred Mwesigye amesema ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini humo kwenda Chongoleani mkoani Tanga, ni shukrani ya nchi hiyo kwa wema wa Tanzania.

Alisema hayo Dar es Salaam alipozungumza katika kipindi cha Good Morning kinachorushwa na kituo cha redio cha Wasafi Media cha Dar es Salaam.

“Sisi na Tanzania si marafiki tu bali ni ndugu wa damu, mlitusaidia sana wakati wa harakati za uhuru na hata baada ya uhuru tuliendelea kuwa ndugu, na ile vita ya Kagera Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa mkombozi wetu,” alisema Balozi Mwesigye.

Alisema awali Uganda ilikuwa chini ya utawala wa Rais Milton Obote na ikaanza vuguvugu la mapinduzi yaliyoratibiwa na wakoloni na kutekelezwa na Idd Amin ambaye aliipindua serikali.

Balozi Mwesigye alikumbusha ambavyo baada ya mapinduzi Uganda, Yoweri Museveni aliyekuwa mwanajeshi, alikimbilia Tanzania na yeye alivyokimbilia Kenya.

Alisema Idd Amin alitaka kuingia Tanzania Nyerere akamuonya na mwaka 1978 akaivamia Kagera na vita ya Kagera ikaanza.

“Hapo ukawa wakati mzuri wa Nyerere kutusaidia, tukakusanyika Tanzania na kupewa usaidizi wa kijeshi na mafunzo huko Morogoro na kisha tukapigana vita tukiwa na Museveni na majeshi ya Tanzania kumuondoa nduli Idd Amin,” alisema Balozi Mwesigye.

Alisema katika mapambano hayo alipangwa kikosi kimoja na Museveni ambaye sasa ni Rais wa Uganda na anawakumbuka baadhi ya wanajeshi wa Tanzania waliopewa idhini na Mwalimu Nyerere kusaidia kupigana vita hiyo kuwa ni Jenerali David Musuguri, Mwita Marwa, Silas Mayunga na Abdallah Twalipo.

Balozi Mwesigye alisema baada ya vita na kuirudisha Uganda kwenye amani, walishindwa jinsi ya kuishukuru Tanzania kwa mchango wake. Alisema baada ya wao kubaini uwepo wa mafuta, wakaona ni vyema warudishe hisani kwa kukubali ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima lijengwe kupitia Tanzania.

“Hatukuwa na njia ya kuishukuru tukajenga shule tatu Tanzania kama shukrani zetu. Lakini hizo hazitoshi, tumebahatika kupata mafuta Uganda tukasema hapana lazima bomba lipite Tanzania kama alama ya shukurani kwa mchango wake kwa Uganda,” alisema Balozi Mwesigye.

Aliishukuru Tanzania kuruhusu ujenzi wa bomba hilo na kusema kelele zinazopigwa kuhusu uharibifu wa mazingira na nyingine hazina msingi kwa sababu sheria na taratibu zote za ujenzi zilizingatia hayo.

“Sisi ni ndugu na mmetuonesha tangu zamani, sio kitendo kidogo ni jambo kubwa na tunashukuru sana, hata mizigo yetu mingi inapita bandari za Tanzania, tunajenga kituo cha kuzalisha umeme katika Mto Kagera, ni ishara ya udugu pia,” alisema Balozi Mwesigye.

Aliongeza, “tunamshukuru sana Mwalimu Nyerere, ile vita tukafanikiwa kumuondoa Idd Amin aliyekuwa amerubuniwa na wakoloni kupindua serikali ya Obote na yeye tukamfukuza na kufanikiwa kushika dola na kujenga serikali.”

Kwa mujibu wa balozi, baada ya Amin kuondolewa, nchi ilikuwa na ukabila na udini hivyo Nyerere akawapa tena baadhi ya viongozi akiwemo Joseph Butiku kwenda kuwasaidia kujenga serikali.

Mwaka 1980, uchaguzi ulifanywa na Rais Obote akashinda na Februari, 1981 waliingia msituni na Museveni kupigana vita kwa miaka mitatu wakamshinda Obote. “Museveni alisoma Tanzania na Mwalimu Nyerere aliona uwezo wake na kusema huyo ni hazina ya baadaye,” anasema.

Balozi Mwesigye alisema Mwalimu Nyerere ni mzazi wa Afrika yote hivyo hawawezi kusahau historia ya uhuru wao wala kuisahau Tanzania.

“Tanzania ni ndugu wa damu, ndio maana ushirikiano wetu tunataka kuuendeleza kuujenga, tunataka vijana wafahamu hilo, kuna umuhimu wa kuwafundisha haya mambo wayajue ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button