Balozi Mongella ajivunia ujasiri, kujiamini kazini
MWANASIASA mkongwe nchini, Balozi Getrude Mongella (78) ameweka wazi safari yake ya uongozi akieleza mambo yaliyomfikisha alipo sasa.
Mongella anajivunia ujasiri na kujiamini kwake kulikomwezesha kufanyakazi kwa ufanisi.
Aidha, Balozi Mongella anaeleza alivyotokwa machozi alipokwenda kuripoti katika ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) baada ya kuteuliwa na Katibu Mkuu wa UN wakati huo Boutros Boutros-Ghali.
Alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (Tanzania Standard Newspapers -TSN) inayochapisha magazeti ya HabariLEO na Daily News pamoja na Daily News Digital.
Mstaafu huyo ni miongoni mwa viongozi ambao waandishi wa TSN wamefanya nao mahojiano yatakayochapishwa kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo maisha na kazi zao.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Dar es Salaam, Mongella maarufu kama ‘Mama Beijing’, anataja mambo makuu yaliyomwezesha kushika nafasi mbalimbali za uongozi ni pamoja na kujiamini, kujitolea, uzalendo na kutoogopa kujifunza.
Jina la Mama Beijing lilitokana na alivyoongoza Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa la Wanawake Beijing, China mwaka wa 1995 akiwa Katibu Mkuu.
Uongozi ni unyenyekevu, kujifunza
Akieleza alivyomudu majukumu yake, alisema zipo aina mbili za uongozi ambazo ni kipaji na kujifunza akisema yeye amekuwa nazo zote.
“Usione aibu kujifunza. Uongozi wa kuchaguliwa au kuteuliwa, unapaswa uwe mnyenyekevu…lazima usikilize mbinu…,” alisemna kuongeza kuwa enzi zake, wanawake wengi hawakujiamini, walizoea kudidimizwa na kujiona hawawezi wakidhani kutojionesha ni sifa.
Akiwa ametunukiwa tuzo zaidi ya 13 ndani na nje ya nchi kuthamini mchango wake katika maeneo mbalimbali, alisisitiza umuhimu wa jamii kulea vipaji vya uongozi miongoni mwa watoto. Mwaka huu amepewa tuzo ya Charlotte Maxeke ambayo ni maalumu kwa wanawake wa Afrika katika diplomasia.
“Kumbe uongozi unahitaji ujitoe, ujioneshe,” alisema Mongella ambaye amefanya kazi na kuongoza taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa, akianza na Uhadhiri wa Chuo cha Ualimu Dar es Salaam mwaka 1970 hadi 1974.
Baada ya hapo, alijiingiza kwenye siasa akianzia mwaka 1975 alipoingia kwenye lililokuwa Bunge la Afrika Mashariki. Miongoni mwa nyadhifa alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Balozi nchini India (1991-1993).
Amewahi kuwa Waziri Asiye na Wizara Maalumu, Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii, Mshauri Maalumu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (Unesco) na Rais wa Bunge la Afrika.
Akimwelezea Rais Samia, Mongella alisema kikazi, si rika lake bali alimfahamu kupitia akina mama waliokuwa walezi wake. Kwa mujibu wa Mongella, katika mkutano wa Beijing, Samia alijitolea kusaidia kundi la mama wazee kutoka Zanzibar.
“Hiki ni kipaji cha kiuongozi. Ilionesha uwazi wake wa kuongoza na kujitolea,” alisema Mongella na kuongeza kuwa vipaji vya Samia vilijionesha wazi zaidi katika Bunge la Katiba kabla ya kuwa Makamu wa Rais.
Akisisitiza umuhimu wa kujiamini, Mongella alisema, “mwanamke ukitamkwa, ili usimame imara kama Mama Samia, ni lazima historia yako iongee.”
Alisema Samia alishika madaraka ya urais katika mazingira magumu, yaliyojaa sintofahamu kutokana na kuwapo watu waliojiuliza kama ataweza na amewathibitishia kuwa ni thabiti kiuongozi.
Akimrejelea Rais Samia kuwa ni mpambanaji, shujaa na anayejiamnini, Mongela, alitoa mfano wa ajenda ya kuwarudisha shuleni watoto waliopata ujauzito na kusema si wote ambao awali waliielewa umuhimu wake.
“Ameingia (Samia) mazingira mazito, ameweza…, tumwombee kwa Mungu kazi iendelee na hili kila mwanamke katika mazingira yoyote, tuwe tayari kuchukua madaraka.”
Mongella alihimiza umma wa Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kumuunga mkono Rais Samia na kumwongezea nguvu ya kuongoza.
“Mwandishi unafanya nini kuhakikisha Rais Samia anaongoza? mna mengi ya kufanya kuhakikisha anaongoza,” alisema na kukemea tabia ya umma kuiangalia serikali kwa kila kitu bila wao kutoa mchango.
Chozi ofisini UN
Akizungumzia uteuzi UN na siku ya kwanza ya kuripoti ofisini, Balozi Mongella alisema kutokana na ukubwa na taratibu za kupamba ofisi, aliogopa kwa hofu na machozi yakamtoka huku akiwaza mazingira aliyoyazoea ya nyumbani Ukerewe.
“Nilipoingia mle ofisini kwa kweli niliogopa na machozi yakanitoka. Kulikuwa na ukuta mmoja mkubwa ambao ulikuwa na ramani ya dunia nzima, nikaangaza macho, akili yangu ikinituma nitafute kwetu Ukerewe ni wapi, nikazungusha akili kwenye ukuta Ukerewe siioni nikaamua kutafuta Tanzania nikaiona,” alisema Dk Mongella.
Balozi Mongella alisema baada ya kuiona Tanzania katika ramani aliamua kutafuta Ziwa Victoria ili azidi kupata faraja ya kuona nyumbani lakini aliona ziwa hilo ni dogo mfano wa nukta.
“Kwa hiyo unapata kazi, nyingine zinakutia hofu na hofu hiyo inaletwa na mambo mengi kwamba nitaweza? Nadhani Rais Samia naye hakupata usingizi, sijui kwamba na sasa analala usingizi,” alisema.
Alifafanua: “Katika utumishi, kuna kazi unaweza kupewa wakati mwingine ukafikiri kuwa imekuzidi kimo lakini usikatae, unaibeba hiyo kazi Mungu atakusaidia utaongoza.”
Wasifu wa Mongella
Mongella ni mwalimu, mwanadiplomasia, mwanaharakati wa haki za wanawake na mwanasiasa ambaye ni vigumu jina lake kuacha kutajwa na yeyote anayezungumzia wanawake maarufu na wenye mchango mkubwa wa maendeleo nchini.
Akiwa ni mwalimu kitaaluma, Mongella ambaye alizaliwa wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza, anasema hakuwa hivyo kwa kubahatisha bali alijengwa na baba yake kabla ya kupata taaluma hiyo mwaka 1970 katika Chuo cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na amekuwa mwalimu wa wengi.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ni miongoni mwa waliosoma naye na alithibitisha hilo mwaka 2011 alipoongoza Jumuiya ya Wanafunzi waliosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuchanga Sh bilioni moja kwa ajili ya chuo hicho.
Museveni alisema Balozi Mongella amekuwa mwalimu wake tangu walipokuwa darasani mwaka 1971 na kuhitimu mwaka 1974.
Kimataifa, Mongella alikuwa Rais wa Kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika mwaka 2004 hadi 2009.
Mama huyu wa watoto watatu, anayeishi eneo la Makongo Juu mkoani Dar es Salaam alizaliwa mwaka 1945 katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza. Baba yake ni Patrice Magologozi na mama yake ni Nambona.