Balozi Rupia kuzikwa kesho Dar

Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Paul Rupia

MWILI wa Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Paul Rupia umewasili jijini Dar es Salaam kutoka Afrika Kusini na unatarajiwa kuzikwa Ijumaa katika makaburi ya Kinondoni.

Mwili huo uliwasili saa 7:00 mchana na kupokelewa na familia, ndugu, mabalozi akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Membe na viongozi wengine wa serikali.

Akizungumza kabla ya mwili huo wa Balozi Rupia kuwasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Balozi Sefue alisema Balozi Rupia alikuwa na mchango mkubwa kwa taifa, Afrika na kimataifa.

Advertisement

“Tumempoteza mtu muhimu aliyekuwa na mchango mkubwa katika utumishi wa umma pamoja na kimataifa. Kwetu sisi alikuwa ni kaka na kiongozi hususani kwa wale aliofanya nao kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwani ndiye aliyekuwa mwenyeji wetu tulipojiunga na wizara hiyo na tulijifunza mengi kutoka kwake,” alisema.

Aidha, alisema kifo cha Balozi Rupia ni pigo kwa wale waliowahi kuwa makatibu wakuu kwa kuwa wamempoteza mshauri. Makatibu wakuu wengine wa zamani ni Marten Lumbanga na Philemon Luhanjo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi Wastaafu (ARTA), Balozi James Msekela alisema ni majonzi na uchungu kumpoteza mwanachama wao ambaye alikuwa ni hazina kwa nchi na kiunganishi cha jumuiya yao na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na serikali kwa ujumla.

Alizaliwa mwaka 1936 mkoani Shinyanga akiwa mtoto wa pili wa mmoja wa wapigania uhuru nchini, mwanasiasa na mfanyabiashara, John Rupia.

Alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi kati ya mwaka 1986 na 1995, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 86 Ijumaa iliyopita Septemba 16 nchini Afrika Kusini alikokwenda kutibiwa.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Joseph Kahama, mwili wa Balozi Rupia utaombewa katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam na kesho utaagwa katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 4:45 asubuhi hadi saa 8:00 mchana utazikwa katika makaburi ya Kinondoni.