BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki leo Alhamisi ameanza ziara katika jimbo la Shandong nchini humo. Mwanadiplomasia huyo anafanya ziara hiyo baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa Serikali ya jimbo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing, Balozi Mbelwa akiwa jimboni humo atazuru katika miji ya Zi Bo, Qingdao na Weihai.
Katika ziara hiyo Balozi anatarajiwa kukutana na viongozi wa miji hiyo pamoja na kushiriki kwenye mikutano ya Kuhamasisha ushirikiano wa na uwekezaji.
Aidha, Balozi atatembelea bandari ya Qingdao ambako bidhaa za kilimo zikiwemo ufuta na soya kutoka Tanzania hupitia, tayari kuingia soko la China.
“Balozi atatembelea viwanda vya kuzalisha zana za kilimo na madini, vifaa tiba, madawa pamoja na vifaa vya ujenzi kielektroniki. Vilevile, Balozi atatembelea na kufanya mazungumzo ya kuanzisha ushirikiano na Chuo cha Ufundi cha ZIBO na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shandong,” imeeleza taarifa hiyo.
Jimbo la Shandong lipo Kaskazini Mashariki mwa China.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022, jimbo hilo lina idadi ya watu milioni 102 na lilishikilia nafasi ya tatu kwa nguvu ya uchumi likiwa na GDP ya Dola za Kimarekani Trilioni 1.3.
Wastani wa pato la mtu mmoja moja (per capital GDP) ilifikia Dola za Kimarekani USD 12,643. Uchumi wa Jimbo hilo unategemea sekta za kilimo ambayo inaongoza katika China nzima ikiwa na mchango wa uzalishaji wa 1/8 ya chakula.
Aidha, sekta ya madini ina mchango mkubwa pamoja na sekta ya viwanda.