Bandari Bukoba wapewa wiki moja kubadilika

MKUU wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ametoa muda wa wiki moja kwa maofisa wa vitengo vinavyosimamia bandari ya Bukoba kuhakikisha wanasimamia vizuri mapato  ya serikali na kujiepusha na mianya ya rushwa.

Chalamila anaendelea kufanya ziara katika tasisi za umma mkoani Kagera na amezungumza na maofisa wasimamizi wa vitengo mbalimbali bandari ya Bukoba na kusema kwa muda mfupi aliokuwepo mkoani Kagera, inaonekana kuna mambo hayaendi vizuri, kuhusu usimamizi katika bandari.

Kutokana na hali hiyo amesema asingependa aanze kwa kugombana, badala yake ametaka wajirekebishe na washirikiane na serikali katika suala la mapato.

“Nimepokea taarifa zenu kuwa usimamizi sio mzuri, naomba pesa ndogo zisitupoteze, kwa sababu serikali imetuamini, hivyo tujiamini na tutimize wajibu wetu.

“Nataka nikirudi hapa siku chache zijazo, mabadiliko yawe yamefanyika, hapo sitacheka na mtu kwa sababu nimeshawaonya, ” alisema Chalamila.

Ofisa wa Bandari ya Bukoba, Denice Mapunda, alisema kuwa kwa sasa kuna mafanikio makubwa ya bandari hiyo, kuchangamka kupokea mizigo mbalimbali kutoka nchi jirani,   ukilinganisha na miaka 5 ya nyuma.

Alisema changamoto kubwa iliyopo ni bandari bubu zinazotumika kutorosha na kuingiza mizigo holela, bila kulipia kodi hasa upande wa visiwani.

Habari Zifananazo

Back to top button