‘Bandari Tanga kuwa ya kimkakati’
SERIKALI imesema inatarajia kuifanya Bandari ya Tanga kuwa ya kimkakati kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kutoka katika nchi za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) na Rwanda.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea na kukagua mradi wa maboresho ya bandari ya Tanga.
Alisema kuwa ameridhishwa na maboresho ya mradi wa ujenzi wa gati hiyo yenye urefu wa meta 450 pamoja na upanuzi wa njia ya kupitisha meli hadi kufika nangani yenye urefu wa kilomita 1.7.
Majaliwa alisema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha maboresho yanayoendelea kwenye Bandari zake hapa nchini yanaweza kuleta tija na manufaa kwa taifa.
Katika hatua nyingine akiwa katika bohari ya mafuta ya GBP aliielekeza EWURA kuangalia namna bora ya wafanyabiashara waliopo Kanda ya Kaskazini kuitumia bohari hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya mafuta.
Alisema kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na mwekezaji huyo ni vema wafanyabiashara wa mafuta katika Kanda hiyo kuitumia Bohari ya GBP kwa ajili ya kupata huduma ya mafuta badala ya kuitumia bandari ya Dar es Salaam.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu hifadhi ya matenki ya GBP, Mkurugenzi Mtendaji wa GBP, Badar Sood alisema ujenzi wa matenki hayo ulianza mwaka 2002 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 25 huku wakipokea meli zenye uwezo wa lita 6,000 tu.
“Hivi sasa tunaweza kuhifadhi lita milioni 200, tunaweza kupokea bidhaa mbili kwa wakati mmoja. Tunapokea hadi meli zenye ujazo wa lita 70,000 na tunaweza kupakia lita milioni tano hadi sita kwa siku kwenye malori na kupakia mabehewa 20 kwa wakati mmoja ndani ya saa tatu,” amesema Badar.
Kwa upande wake Naibu Mkurungenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini TPA Juma Kijavara alisema kuwa maboresho ya mradi huo yamefikia asilimia 99.
Alisema kuwa kutokana na maboresho hayo uwezo wa kuhifadhi shehena ya makasha umeongezeka maradufu tofauti na hapo awali.
“Kutokana na kuongezeka kwa mizigo ya makasha tupo kwenye mpango wa maboresho ya kujenga miundombinu mingine kwa ajili ya kuongeza eneo la kuhifadhi makasha katika eneo la maghala ya kuhifadhi mizigo,” alisema Kijavara.
Naye Mkuu wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba alisema kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji ndani ya mkoa huo yameanza kuleta matokeo mazuri kwani viwanda vimeweza kuongezeka kutoka 16 hadi 25.
Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu aliiomba serikali kufuata maagizo ya Bunge ya kuitaka mikoa ya Kaskazini kuitumia bohari ya mafuta ya GBP kwa ajili ya kuchukulia mafuta.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda cha saruji cha Maweni na kupokea taarifa ya ujenzi wake unafanywa na kampuni ya HUAXIN ya China.