Bandari ya Dar es salaam kupokea meli kubwa zaidi

DAR ES SALAAM: MABORESHO makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, yameiwezesha bandari hiyo kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa na za kisasa zenye urefu hadi kufikia  mita 305.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kuhusu uwezo wa bandari hiyo, mara baada kukamilika kwa ukarabati wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema kwa sasa ipo tayari kwa ajili ya kuhudumia meli za aina hiyo kwa ufanisi.

“Kabla ya ukarabati huo, bandari hiyo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu wa mita zisizozidi 250 na ikitokea ikiingiza meli kubwa zaidi hazizidi mita 300,” amesema

Advertisement

Aidha, amesema wameongeza kina cha maji na kuimarisha zaidi magati  kwa sasa yana uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na zenye urefu mkubwa kwa ufanisi.

“Kwa sasa, Bandari ya Dar es Salaam imeboresha magati yake na kuongeza kina kwenye magati hayo hadi kufikia urefu wa mita 14.5 kwenye gati namba 1 hadi 7,” amesema

Mbali ya kuboreshwa kwa magati hayo, eneo la kugeuzia meli limeongezwa upana hadi kufikia mita 520 ili kuwezesha meli za kubwa zaidi kuingia bandarini kwa urahisi.

Pia amesema wameboresha lango kuu la kuingia bandarini pia limechimbwa na kuwa na urefu wa kina cha mita 15.5 pamoja na upana wa mita 200.

Bandari ya Dar es Salaam ni moja kati ya bandari mama zinazoendeshwa na kumilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania. Bandari nyingine ni pamoja na Bandari za Tanga na Mtwara.