Bandari ya Kabwe inavyorahisisha usafirishaji mizigo Ziwa Tanganyika

USAFIRISHAJI wa mizigo na abiria kupitia Bandari ya Kabwe iliyopo Nkasi mkoani Rukwa umewavutia wafanyabiashara kutokana na kupunguza gharama na kurahisisha usafirishaji ikilinganishwa na sekta nyingine kama barabara.

Kabla ya ukarabati wa bandari hiyo, wafanyabiashara walikuwa wakitumia barabara kusafirisha mizigo na kuwalazimu kutumia gharama kubwa na wakati mwingine kulipa gharama za uharibifu kutokana na mizigo kuharibika.

Vumilia Salum, ambaye ni mnunuzi wa mihogo kutoka Wilaya ya Nkasi na kuiuza katika masoko ya Mkoa wa Kigoma kwa muda wa miaka kumi sasa anasema awali alipokuwa akisafirisha bidhaa zake kwa njia ya barabara alikuwa akitumia gharama kubwa akilinganisha na njia ya maji.

Anasema ili bandari hiyo iendelee kutoa huduma nzuri na endelevu kwao na wateja wao, serikali inapaswa kuendelea kufanyia maboresho ya mara kwa mara bandari hiyo ili kuifanya iendelee kutoa huduma hiyo.

“Nipo kwenye hii biashara kwa miaka kumi sasa. Tunaishukuru sana serikali kwa ujenzi wa bandari hii ambao umerahisisha biashara zetu. Huko nyuma nilikuwa natumia gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zangu kwa kutumia malori ya mizigo, lakini baada ya kuanza kutumia haya mashua nimeona utofauti mkubwa kwenye gharama,” alisema Vumilia.

Mmiliki wa malori, Suleiman Mohamed ambaye anasafirisha mizigo kutoka Bandari ya Kabwe kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anasema ujenzi wa bandari ya Kabwe umekuwa ni mkombozi kwao kibiashara lakini changamoto iliyobaki ni ubovu wa barabara inayoingia bandarini hapo na kutaka serikali iifanyie maboresho.

“Kwa kweli huduma ni nzuri kwetu na biashara inakwenda vizuri. Lakini tunaomba mamlaka zinazohusika na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kuiboresha barabara inayotoka Barabara Kuu ya Katavi-Rukwa kuja hapa bandarini ili biashara ikue zaidi,” alisema mfanyabiashara huyo.

Aidha, Mohamed aliomba mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya usafirishaji bidhaa kwenda Congo zitoe vibali hivyo haraka kwao ili kuwaepusha na gharama kubwa za kufanya biashara wanazoingiza kutokana na ucheleweshaji wa vibali hivyo.

Ujenzi wa Bandari ya Kabwe umekuwa ni chachu ya ukuaji uchumi katika Mkoa wa Rukwa baada ya kukuza biashara ndani ya mkoa huo na nchi jirani za DRC na Burundi.

Aidha, ndiyo lango kuu kwa wafanyabiashara wa mihogo, mahindi, mchele, sukari wanaosafirisha bidhaa hizo kutoka bandari ya Kalemie kwenda katika Bandari ya Kalemie na Moba za nchini Congo.

“Wafanyabiashara wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania sasa wanakuja kununua mazao ya chakula kutoka kwetu na kuyasafirisha kwenda nchi za Congo, Burundi na Kigoma na kufanya mzunguko wa pesa kuongezeka na kubadilisha maisha yetu lakini huko nyuma biashara ilikuwa ngumu,” alisema Julius Kagosha, mkulima wa mahindi na mihogo, Nkasi, Mkoa wa Rukwa.

Alisema kabla ya ujenzi wa bandari ya Kabwe wakulima hasa wa mahindi na mihogo walikuwa na changamoto ya kibiashara ya mazao hayo kutokana na wafanyabiashara wengi wanaosafirisha bidhaa za mazao nchi za DRC, Burundi na Mkoa wa Kigoma kwenda mjini Sumbawanga kununua mazao hayo kwa sababu walikuwa wakitumia njia ya barabara kutoka mjini humo kwenda mikoa ya mwambao wa Ziwa Tanganyika na nje ya nchi.

Anasema wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa za mazao kwenda nchi jirani za Congo walikuwa wakifuata bidhaa hizo Sumbawanga mjini na kuzisafirisha kwenda Kigoma katika bandari za Kigoma na Kibirizi kabla ya kuzisafirisha kwenda kwenye nchi hizo na kufanya gharama za usafirishaji kuwa kubwa.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu wa ujenzi wa Bandari ya Kabwe kwa kuwa sasa mazao yetu yamepata soko kubwa na sasa sisi wakulima hatuna tena changamoto bei ya mazao yetu na pia wapi tuyauze,” alisema Kagosha, mkulima wa mahindi na mihogo.

Bandari ya Kabwe ambayo ujenzi wake ulianza mwezi Aprili 2, 2018 na kukabidhiwa rasmi kwa Serikali Aprili 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 7.49 ni miongoni mwa bandari za mwambao wa Ziwa Tanganyika zilizokuwa kwenye orodha ya Mradi wa Serikali wa uboreshaji wa bandari za maziwa makuu nchini kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Kabwe ulihusisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu ya bandari ikiwemo ghala la kuhifadhia mizigo, jengo la abiria na ofisi mbalimbali zilizofanyiwa marekebisho na gati lenye kina chenye urefu wa meta 5.5 ambalo linaruhusu boti kubwa kutia nanga bandarini hapo.

Inamchukua mfanyabiashara takribani saa 6 mpaka 7 kusafirisha bidhaa zake kutoka bandari ya Kabwe mpaka kufika bandari maarufu ya Kalemie nchini Congo kupitia Ziwa Tanganyika kutokana na ukaribu wa bandari hizo kijiografia na kuifanya kuwa bandari ya pili kwa kufanya vizuri kibiashara baada ya bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma.

Bandari ya Kabwe ambayo inatoza Sh 7,000 kwa tani ambayo ni tozo nafuu zaidi iliyowekwa na TPA inahudumia hadi tani 1,200 ya shehena na abiria 400 kwa mwezi na kwa asilimia kubwa ni katika nchi ya DRC.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula anasema TPA imeweka tozo za nafuu kwa wateja wake katika bandari ya Kabwe ili kufanya mazingira ya biashara kuwa rafiki ili kuwafanya waendelee kutumia bandari hiyo katika mazingira mazuri na wezeshi kwao.

Aidha, alisema bandari hiyo imeweka mazingira mazuri ya usalama na ulinzi kwa wafanyabiashara, abiria na mali zao na kurejea azma ya TPA ya kujenga bandari zaidi za kisasa nchini na kutoa huduma bora kwa wateja wake.

“Tumeweka tozo za chini kwa wateja wetu katika bandari hii ili kufanya mazingira ya biashara kuwa rafiki na kuwafanya waendelee kuitumia bandari katika mazingira mazuri na wezeshi kwao. Bandari imeweka mazingira mazuri ya usalama na ulinzi kwa wafanyabiashara wetu, abiria na mali zao ikiwa ni azma ya TPA ya kujenga bandari zaidi za kisasa nchini na kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” alisema Mabula.

Awali kabla ya ujenzi wa bandari ya Kabwe wafanyabiashara walilazimika kutumia mitumbwi midogo kusafirisha bidhaa zao kupitia bandari bubu zisizo rasmi zilizopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bandari hii mpya, boti kubwa zenye uwezo wa kubeba shehena kubwa za mizigo zilianza kutia nanga bandarini hapo na kufanya biashara baina ya Tanzania hasa katika Mji wa Nkasi na nchi jirani za DRC na Burundi kukua.

Licha ya umuhimu mkubwa wa bandari ya Kabwe kwa maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa hususani Wilaya ya Nkasi iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, bado inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara inayoingia bandarini hapo kutoka mjini Sumbawanga ambayo kama itakarabatiwa kwa kiwango cha lami, biashara katika bandari hiyo itakua maradufu ikilinganishwa na sasa.

Suleiman Mohamed ambaye ni mmiliki wa malori ya mizigo anayesafirisha mizigo kutoka bandari ya Kabwe kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema ujenzi wa bandari ya Kabwe umekuwa ni mkombozi kwao kibiashara lakini changamoto iliyobaki ni ubovu wa barabara inayoingia bandarini hapo na kutaka serikali iifanyie maboresho.

“Kwa kweli huduma ni nzuri kwetu na biashara inakwenda vizuri. Lakini tunaomba mamlaka zinazohusika na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kuiboresha barabara inayotoka Barabara Kuu ya Katavi-Rukwa kuja hapa bandarini ili biashara ikue zaidi,” alisema mfanyabiashara huyo.

Aidha, Mohamed aliomba mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya usafirishaji bidhaa kwenda DRC zitoe vibali hivyo haraka kwao ili kuwaepusha na gharama kubwa za kufanya biashara wanazoingia kutokana na ucheleweshaji wa vibali hivyo.

Habari Zifananazo

Back to top button