Bandari ya Karema yaanza kufanya kazi

Mradi mkubwa wa kimkakati wa bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi sasa rasmi umeanza kufanya kazi jana Septemba mosi 2022,ukiwa na manufaa makubwa nchini hususani kwa wafanyabiashara na wasafiri wanaotumia mwambao wa ziwa Tanganyika.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2019 na kukamilika mwaka 2022 kwa zaidi ya Tsh.

Bilioni 47 ni lango linalounganisha nchi ya DR Congo na Tanzania katika mambo mbalimbali ikiwemo uchumi ,kilimo na masuala ya usafirishaji.

Akizungumza baada ya kushuhudia bandari hiyo ikifanya kazi Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amezitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kushawishi na kuratibu meli za kutoka Kasanga DR Congo, Zambia na Burundi kuanza kutia nanga katika Bandari ya Karema.

“Bandari iko tayari,TPA na TASAC popote mlipo hakikisheni mnaratibu meli kubwa za kuja hapa wakati serikali inatengeneza meli ambazo zitakuwa za kisasa”amesema DC Buswelu

Kwa upande wake mwakilishi wa meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa Tanganyika Fikiri Musiba amesema wamepokea abiria 35 pamoja na boti inayoshughulika na masuala ya kutalii huku akiahidi kuitunza na kuzingatia matumizi sahihi ya bandari hiyo.

Meneja Mamlaka ya mapato Mkoa wa Katavi (TRA) Jacob Mtemang’ombe amewataka wafanyabiashara kuachana na Bandari zisizo rasmi ili kukwepa kodi na badala yake kutumia Bandari hiyo.

Kwa upande wa baadhi ya abiria walioshuka katika Bandari hiyo wameishukuru serikali kuwekeza mradi huo hadi kukamilika kwani awali maisha yao yalikuwa hatarini kutokana na kutokuwa na usafiri wa uhakika hasa wa meli kubwa kutokana na kukosekana usafiri wa uhakika.

Bandari hiyo ya Karema inatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

Back to top button