Bao limegoma Uwanja wa Amaan
ZANZIBAR: Bado hakuna bao katika Uwanja wa Amaan Zanzibar ( New Amaan Complex)
Tayari michezo mitatu imepigwa katika uwanja huo tangu ulipozinduliwa Desemba 27, 2023 baada ya kufanyika ukarabati mkubwa na kuufanya kuwa na muonekano wa kisasa zaidi.
Ikumbukwe siku ya uzinduzi wa dimba hilo moja ya wadau wa michezo aliahidi kutoa zawadi ya Sh milioni moja kwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika uwanja huo na mpaka sasa mambo yamekuwa magumu.
Mchezo kwa kwanza Zanzibar Heroes na Kilimanjoro Stars ulimalizika 0-0 pia mchezo wa pili ambao ulikuwa ni wa ufunguzi wa Michuano ya Mapinduzi, Mlandege vs Azam Fc ulimalizika bila bao kupatikana kama ilivyokuwa pia katika mchezo wa tatu Chipukizi dhidi ya Vital‘o FC ya Burundi.
Macho yanaelekezwa kwenye michezo miwili ya leo labda linaweza kupatikana bao la kwanza katika uwanja huo ambapo KVZ FC watavaana na Jamhuri SC kisha JKU SC watapapatuana na Singida FG.