Barabara Hifadhi  ya Ruaha yawaibua tena wadau

WADAU wa utalii wameendelea kuiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya lami kuelekea hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ubovu wake kwa miaka yote umeelezwa kuwa moja ya sababu inayoikosesha hifadhi hiyo watalii na mapato ya kutosha.

Pamoja na hifadhi hiyo kuwa ya pili kwa ukubwa baada ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikiwa na kilometa za mraba zaidi ya 20,000 taarifa za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) zinaonesha pamoja na ukubwa huo inategemea sehemu ya mapato kutoka hifadhi za kaskazini ili kujiendesha.

Hifadhi hiyo iliyopo kilometa 131 kutoka Iringa Mjini ni maarufu kwa idadi kubwa ya Tembo, kudu wakubwa na wadogo, pofu, simba, chui, nyati, pundamilia, mbweha, fisi, mbwa mwitu, twiga, swala pala, ndege zaidi ya 500 na mimea karibu yote inayopatikana kusini na mashariki mwa Afrika.

Imepewa jina hilo kutokana na mto Ruaha Mkuu wenye samaki za aina mbalimbali, viboko na mamba kupita ndani yake; mto huo ndio tegemeo kubwa la maji kwa wanyama hasa katika kipindi cha kiangazi.

Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji watalii ya Safi Tours and Safari, Roy Mahimbi amesema; “Miundombinu ya barabara ya kutoka Iringa Mjini hadi hifadhini ni mibovu, inadhoofisha utalii wa kusini na kuwakimbiza watalii wengi hususani wazee.”

Alisema gari zao zimekuwa zikitumia muda mrefu kusafirisha watalii na zimekuwa zikiumia na kuharibika mara kwa mara katika barabara hiyo ambayo ahadi yake ya kujengwa kwa kiwango cha lami ni ya miaka mingi.

“Utalii ni starehe, sio mateso; watalii wanataka kusafiri kwa raha na wakati mwingine kwa muda mfupi kutoka kituo kimoja kwenda kingine, wengi wao wanakimbili hifadhi za kaskazini kwa sababu miundombinu ya barabara na usafiri wa anga imeimarishwa,” alisema.

Akiiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo, Mahimbi alisema ikijengwa kwa lami itavutia watalii wengi wakiwemo wale wa ndani wanaoshindwa kuitembelea kwa kutumia magari yao kwa sababu ya ubovu wake.

Aidha aliomba serikali na wadau wengine wa utalii kutumia kampuni za usafirishaji watalii zilizosajiliwa ili ziendelee kutoa ajira kwa watanzania wengi, na zikue na kukuza mapato ya serikali na sekta yenyewe.

Pamoja na ombi hilo, wadau hao wamekiri kufurahishwa na ukarabati wa uwanja wa Ndege wa Iringa unaotarajiwa kukamilika na kuanza kupokea ndege kubwa aina ya Bombardier baada ya Agosti 26, mwaka huu.

Mkurugenzi wa hoteli ya Mabata Makali Lodge and Campsite, Eward Athanas aliipongeza serikali kwa kuja na mikakati inayolenga kutangaza utalii kusini mwa Tanzania kupitia mipango mbalimbali ukiwemo Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

“Ni matarajio yetu kuwa, utekelezaji wa mikakati hii utaongeza idadi ya watalii wanaotembelea ukanda huu hivyo, ongezeko la ajira na fursa za uwekezaji, na mapato ya serikali na ya mwananchi mmoja mmoja,” alisema Athanas.

Wakati Uwanja wa Ndege wa Iringa ni muhimu kwa ajili ya kurahisishaa huduma za usafiri katika ukanda huo, alisema barabara ya lami itaongeza hamasa kwa watalii wa ndani hususani wa mikoa ya jirani kuitembelea mara kwa mara hifadhi hiyo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo hivikaribuni, Meneja wa Mkoa wa Iringa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Daniel Kindole alisema ukarabati wa uwanja wa Ndege Iringa kwa zaidi ya Sh Bilioni 63.7 unaendelea na utakamilika na kuanza kutoa huduma Agosti mwaka huu kama ilivyopangwa.

“Ujenzi huo unahusisha njia mpya ya kutua na kuruka ndege, maegesho ya ndege, njia ya mchepuo wa ndege, jengo la zimamoto na kituo cha nishati, kuweka taa za ardhini na ujenzi wa jengo la abiria la muda,” alisema.

Kuhusu barabara ya lami kuelekea hifadhi ya Taifa ya Ruaha, alisema kazi ya kuhuisha taarifa za watu watakaothiriwa na ujenzi kwa lengo la kuwalipa fidia unaendelea sambamba na maandalizi ya manunuzi kwa ajili ya ujenzi wake.

Habari Zifananazo

Back to top button