Barabara Karagwe-Burigi Chato kukamilika Novemba

BARABARA ya kimkakati ya Karagwe kupitia Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato kilometa 60 inayotegemewa kwa usafirishaji wa mizigo katika nchi za Afrika Mashariki inatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Akiwasilisha taarifa katika kikao cha bodi ya barabara kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za barabara na mpango wa bajeti mwaka wa fedha 2024/2025, Meneja wa TANROAD Mkoa wa Kagera, Ntuli Mwaikosesy amesema barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami itagharimu Sh bilioni 92 na mradi umefikia asilimia  33.

Alisema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi wa China Road And Bridge Corporation kutoka China ambapo malengo yaliyokuwa yamepangwa ni kuwa mradi huo ungekuwa umefikia asilimia 68 hivyo wako nyuma asilimia 34.

Alisema kuwa moja ya changamoto iliyokwamisha mradi huo ni ulipaji wa fidia ambapo kwa sasa serikali imetatua changamoto hiyo kwa kulipa fidia kiasi cha Sh bilioni 2.7 kwa wananchi zaidi ya 600 hivyo mradi unaendelea kutekelezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Tanroad katika kuhakikisha mradi huo unaendelea kutekelezwa mkoani Kagera na kuwataka wakandarasi  kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza mradi huo kwa wakati.

Alisema kuwa mradi huo ukikamilika licha ya kutegemewa sana na nchi za Afrika Mashariki  katika maswala ya usafirishaji bado  barabara hiyo itatumika katika shughuli za utalii na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja katika Wilaya ya Karagwe.

Wakala wa barabara TANROAD Mkoa wa Kagera imewasilisha bajeti yake ya matengenezo  kiasi cha Shi  bilioni 12.594 na bajeti ya miradi ya  maendeleo Sh bilioni 7.79  kwa mwaka wa fedha  2024/2025.

Habari Zifananazo

Back to top button