NAIBU Waziri wa Ujenzi, Injinia Godfrey Kasekenya amesema Serikali inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Rungwa – Mkiwa (km 503.36) kwa awamu ambapo sehemu ya Mbeya – Chunya – Makongolosi (km 111) ujenzi umekamilika.
Kasekenya amesema hayo leo Februari 5, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka aliyeuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Makongolosi – Rungwa.
“Ujenzi wa sehemu ya Noranga – Itigi – Mkiwa (km 56.9) sehemu ya Noranga – Itigi (Mlongaji) (km 25.) umefikia asilimia 72 na kwa sehemu ya Noranga – Doroto (km 6) na Itigi – Mkiwa (km 25.6) kazi ya ujenzi zimeanza na utekelezaji wa mradi unaendelea”. amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya ameongeza kuwa sehemu iliyobaki ya barabara ya Makongolosi – Rungwa – Noranga (km 356) Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi.
Kuhusu upanuzi wa barabara ya Moshi – Arusha eneo la Kikavu, Kasekenya amesema taratibu za manunuzi zinaendelea kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).