Barabara ya kulipia yaja, sekta binafsi TRC, Tazara

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imesema inajipanga kubadilisha sheria ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika huduma ya usafi ri wa reli kwa kununua mabehewa na kuyaendesha.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameyasema hayo wakati anafungua Mkutano wa 15 wa Mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi.

Profesa Mbarawa alisema ushiriki wa sekta binafsi, serikali na wadau wa maendeleo utaharakisha ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege na meli na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kuhuisha miundombinu ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

“Serikali tumejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara mpya ya Kibaha-Chalinze Morogoro kilometa 215 (express way), ambapo mkandarasi atajenga kwa fedha yake na watakaotumia barabara hiyo watalipia,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema ni muhimu Tanzania iwe na miundombinu bora ili kumudu kuhudumia soko la ndani na nchi sita ambazo hutegemea huduma ya uchukuzi kutoka Tanzania, ambazo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Kingdom Mbangula alisema barabara mpya ya kulipia itakuwa na njia nne, mbili kwenda Morogoro na mbili kurudi Kibaha na magari hayatapishana ili kuepusha msongamano na ajali.

“Tanroads tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mradi huu unajengwa kwa ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati,” alisema Mbangula.

Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Patricia Laverley aliishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuandaa mkutano huo wa tathmini wa kila mwaka ambao unaibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

Dk Laverley alisema AfDB imetenga asilimia 60 ya bajeti yake katika uwezeshaji ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika.

Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire alisema mkutano huo utaibua hoja zinazolenga kuboresha sekta ya uchukuzi hivyo kuvutia wawekezaji wengi kupitisha mizigo yao Tanzania na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x