Barabara ya Mlima Kitonga kupanuliwa
HATIMAYE serikali imesikia kilio cha Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa cha kufanya upanuzi wa barabara katika mlima wa Kitonga, wilayani Kilolo mkoani humo.
Kwa muda mrefu kamati hiyo inayoongozwa na Salim Asas imekuwa ikiiomba serikali ama kupanua barabara hiyo au kujenga barabara nyingine ya mchepuo ili kupunguza ajali na foleni ya magari yanayosafiri ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo ametembelea barabara hiyo yenye mlima mkali na akatoa taarifa ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya upanuzi huo.
Katika ziara hiyo aliyoambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani, viongozi wa chama na serikali na wabunge, Bashungwa amesema serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 6.4 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ikiwa ni suluhisho la muda mfupi la kukabiliana na changamoto hizo katika mlima huo.
“Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kwa maendeleo ya sektaya usafirishaji na uchumi wa nchi.
Ni barabara iliyopo katika mipango yetu na tuahidi kwamba changamoto zake zitaendela kufanyiwa kazi,” alisema.
Awali Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa, Mhadisi Yudas Msangi alisema kwa kutumia fedha hizo jumla ya mita 1600 za Mlima Kitonga zitatanuliwa ili kupunguza foleni na ajali katika eneo hilo la barabara hiyo ya Tanzania Zambia (TANZAM).
Mhandisi Msangi alizungumzia suluhusho la muda mrefu la barabara hiyo akisema Oktoba 3, mwaka huu Tanroads ilisaini mkataba wa usanifu wa kina wa upanuzi wa Mlima Kitonga.
“Hadidu za rejea za mradi huu zinamtaka mhandisi mshauri kuona uwezekano wa kupata njia mbadala ya kudumu inayokadiriwa kuwa ya kilometa 31 itakayopita katika vijiji vya Mlowa, Mifugo, Mlafu na Ilula ili kupunguza changamoto katika mlima huo,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas aliishukuru serikali kwa kusikia kilio cha kamati yake akisema lengo lao ni kufanya barabara za mkoa wa Iringa zipitike wakati wote na kwa usalama.
Asas alizungumzia changamoto za barabara hiyo akisema barabara pana zinaweza kuwa na njia nyingi za kuingia na kutoka, na kuongeza nafasi ya kuona magari mengine hatua inayoweza kupunguza hatari ya ajali na foleni.
Pamoja na kushukuru kwa mpango huo, Asas alisema ni muhimi ikazingatiwa kuwa kupanua barabara pekee haitoshi kuzuia ajali.
“Elimu ya usalama wa barabarani, utekelezaji wa sheria za barabarani, na utunzaji wa magari ni muhimu pia katika kuboresha usalama wa barabarani,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego kwa upande wake amesema kuboreshwa kwa barabara hiyo kutachochea utalii kusini mwa Tanzania.