Barabara ya mwendokasi Kibaha- Dodoma yaja

MOROGORO: WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema mipango ya serikali ya awamu ya sita ni kujenga barabara ya mwendokasi ( Express way) kuanzia Kibaha- Chalinze – Morogoro mpaka makao makuu ya nchi Dodoma.

Bashungwa amesema hayo wakati akizugumza na waandishi wa habari alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kabla ya kuanza ziara yake ya siku nne katika mkoa huo.

Waziri Bashungwa amesema kujengwa kwa barabara ya mwendokasi kutoka Kibaha ambako barabara hiyo imeishika kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha ipo katika mipango ya serikali.

Waziri Bashungwa amesema katika maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hasaan kwenye barabara ni kuona Dar es Salaam kama mji wa kibiashara unainganishwa kupitia Morogoro na makao makuu ya nchi Dodoma.

Bashungwa amesema pia Rais kupitia wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Profesa Makame Mbarawa kwa upande wa Reli ya Mwendokasi (SGR) kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma na maeneo mengine ya nchi yanaunganishwa na Reli hiyo .

“Utaangalia upande mmoja kuna SGR na upande mwingine kuna barabara ya mwendokasi inayounganisha Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma na kwa wana Morogoro hii ni neema kubwa kwa sababu shughuli za kilimo zitazidi kushamiri “amesema Bashungwa.

Bashungwa amesema ,Mkoa wa Morogoro una wakulima hodari na kwenye kikapu cha mchango wa Taifa kwenye uzalishaji wa chakula , mkoa huo una mchango wake  ni mkubwa.

“Ni maelekezo ya Rais kwa vile Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati kwenye kilimo …maelekezo yake ni kuendelea kuiunganisha Morogoro na dunia kwa kuboresha miundmbinu ya barabara “ amesema Bashungwa.

Bashungwa amesema kila mkulima wa Mkoa wa Morogoro atajivunia ya kwamba akilima mazao yake anajua kuna miundombinu bora ya  usafirishaji kwa kutumia reli ya mwendokasi au kwa njia ya barabara  .

Waziri Bashungwa amesema maboresho hayo pia yanafanyika kwenye  viwanja vya ndege kikiwemo cha Dodoma ambazo kinaendelea  kukamilishwa  pamoja na  kiwanja cha mkoani  Iringa.

“ Naiona Morogoro ya kesho ni Morogoro ambayo imekaa kimkakati na Rais Dk Samia anazidi kuboresha miundombinu  ili mkoa huu uzidi kuwa mkoa wa kimkakati katika kuendelea kusaidia uchumi wan chi kupitia kilimo “ amesema Bashungwa.

Habari Zifananazo

Back to top button