KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo amekerwa na ubovu wa Barabara ya Orbesh -Haydom,wilayani hapa mkoani Manyara ambayo inapitika kwa tabu na imepigiwa kelele muda mrefu kuombwa itengenezwe.
Kauli hiyo ameitoa leo Kata ya Hyderer wilayani hapa, wakati akisikiliza kero za wananchi na akizungumza nao pamoja na wanachama wa CCM.
“Hatuko tayari kuona mambo yanachelewa ilihali tuliwaahidi wananchi kujenga barabara hii, Waziri wa ujenzi bado hajashugulika na miundimbinu Manyara,”amesema Chongolo.
Awali Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay akizungumza kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, amesema licha ya kuipigia kelele barabara hiyo bado hadi sasa mkandarasi hajapewa hata senti moja kuanza ujenzi wa Km 25 za awali.
Akizungumzia barabara hiyo, Chongolo amesema, mbunge huyo alishapiga sarakasi bungeni akisisitiza ujenzi wa barabara hiyo, lakini hadi sasa haijachukuliwa hatua na ni kero na hajafurahishwa na hali yake.
“Mbunge huna haja ya kuruka sarakasi tena nitaibeba mimi, hatuna sababu ya kuwa na viongozi wasiotimiza wajibu wao, sijafurahishwa na barabara hii, nimeipita leo ni mbaya,” amesema Chongolo.