“Baraza la Ardhi Maswa kesi zinaendeshwa miezi 21”

SIMIYU: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu imesema kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 ilifanya chambuzi tano za mfumo wa utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi.

Uchambuzi wa mifumo hiyo umefanyika kupitia mabaraza ya ardhi na nyumba yaliyopo mkoani humo, ambapo ilibainika ucheleweshwaji wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye Baraza la ardhi na nyumba katika Wilaya ya Maswa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo, Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa, Aron Misanga amesema katika Baraza hilo walibaini mashauri kuendeshwa kwa muda wa miezi 21.6.

“ Kwa mfano tulikutana na moja ya shauri kwenye hilo Baraza la Wilaya ya Maswa ambalo lilikuwa bado halijatolewa uamuzi, shauri hilo lilikuwa limeendeshwa kwa muda miaka mitano na bado uamuzi ulikuwa haujatolewa,” amesema Misanga.

Amesema kuwa moja ya changamoto ambayo ilikutwa kwenye Baraza hilo, ni uchache wa watumishi, lakini pia Baraza hilo kupokea mashauri mengi kutoka maeneo mengi ya Mkoa wa Simiyu.

“ Mkoa wa Simiyu una mabaraza mawili tu, Maswa pamoja na Busega, wilaya nyingine za Bariadi, Itilima, Meatu hazina Mabaraza hivyo…Baraza la Maswa linajikuta linapokea kesi nyingi kushinda uwezo wake” alisema Misanga.

Aidha Naibu Mkuu huyo wa Takukuru, amesema kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo la Maswa ndiye anahusika kuendesha Baraza la Busega hali ambayo nayo walibaini inachelewesha kesi nyingi kushindwa kutolewa uamuzi haraka.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button